Matumaini Yetu Wachezaji Wako Tayari Kufanya Vizuri; Shime
Kauli ya kocha mkuu wa timu za Taifa za wanawake Bakari Shime akizungumzia maandalizi ya kikosi cha U17 Machi 3, 2022 walipokuwa mazoezini kwenye uwanja wa Amaan.
Kikosi hicho kinachojiandaa kwa mchezo wa kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Botswana , unaotarajiwa kuchezwa Machi 6, 2022 kwenye uwanja wa Amaan huko visiwani Zanzibar.
Shime amesema kuwa wapo kwenye hatua za mwisho za maandalizi na kwamba wanaamini wachezaji wako tayari kufanya vizuri kwenye mashindano hayo, licha ya kuwa wanategemea mchezo huo hautakuwa rahisi kutokana na kuwa ndio mechi zao za hatua ya kwanza kwenye mashindano hivyo wote hawajapata nafasi ya kusomana.
Alisema hali ya kikosi kwa ujumla ni nzuri na kwamba hakuna majeruhi yeyote wachezaji wapo kwenye hari nzuri pamoja na kupokea maelekezo vile wanavyo elekezwa na waalimu wao,” Tunaimani kubwa na wale ambao watachaguliwa kuanza kuipeperusha bendera ya nchi kwenye mchezo huo kuwa watafanya vizuri, tofauti na hapo mengine ni ya uwanjani”. Kauli ya kocha Shime
Hata hivyo kocha amesisitiza swala zima la sapoti kwa timu za Taifa hususani kwa wanawake kuweza kuzishika mkono timu za Taifa kwa upande wa wanawake ikiwa ni katika kuunga mkono juhudi za Serikali na TFF kuzifikisha mahala pazuri timu hizo, hasa zinaposhiriki mashindano ya namna hiyo.
Mara baada ya mchezo huo wa Machi 6, 2022 uwanja wa Amaan, kikosi cha U17 kitakuwa na kibarua kingine cha kuwafuata Botswana kwenye mchezo wa marudiano ambao pia utachezwa mwezi Machi mwaka huu.