Kazi ya Serikali ni Kuweka Mazingira Wezeshi kwa Timu Zote Zinazo Peperusha Bendera

 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa  Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa Disemba 21, 2021 alipokutana na timu ya Taifa ya Tanzanite pamoja na benchi la ufundi kwa ujumla ili kuweza kuzungumzia na kufanya tathmini ya changamoto mbalimbali za kimichezo zilizo jitokeza nchini Burundi kwenye mchezo wa marudiano baina ya Tanzanite na timu ya Taifa ya Wasichana chini ya miaka 20 nchini humo.

Waziri Bashungwa alisema kuwa kazi ya Serikali katika sekta ya michezo ni kuweka mazingira wezeshi kwa wanamichezo na timu zote zinazo peperusha bendera ya Taifa, na ndoto ya serikali ni kuwaona wachezaji na timu zao wakiibuka washindi katika kila mchezo.

Sambamba na hayo Waziri Bashungwa ameipongeza pia timu ya Tanzanite kwa  matokeo ya sare (1-1) waliyoyapata Disemba 18, 2021 wakiwa ugenini na kufanikiwa kuwaondosha Burundi huku wao wakiendelea mbele na hatua nyingine kwenye mashindano hayo.

Akizungumza Kocha mkuu wa timu ya Tanzanite Bakari Shime changamoto walizo kutana nazo mpaka kumalizika kwa mchezo huo, alisema kuwa changamoto zilianzia nyumbani baada ya kuchelewa kupata ndege itakayo weza kukidhi kusafirisha wachezaji wote lakini pia kuchelewa kwa majibu ya Uviko 19. Hali iliyopelekea kuwapunguza morali wachezaji mapema zaidi.

Aidha kocha Shime aliongeza kuwa ugumu zaidi ulitokea wakiwa nchini Burundi baada ya kufanikisha zoezi la wachezaji wote kufika eneo la mchezo, “Shida ilianzia kwenye majibu ya Covid-19 ambapo tuliambiwa wachezaji 9 ni positive na baada ya muda wakabadilisha na kusema wachezaji wote positive kisha yakaja majibu mengine yaliyoruhusu wachezaji 8 pekee ambapo kati yao alikuwepo mlinda mlango mmoja”.

Kocha alisema kuwa licha ya kikosi chake kucheza kikiwa pungufu (8) kulinganisha na wapinzani wao ambao walicheza wakiwa kamili bado haikuwa ngumu kwao kujituma na kuipambania bendera ya nchi na hatimaye kupata bao la kuongoza kabla ya Burundi kusawazisha bao hilo, matokeo yaliyo salia hivyo mpaka kumalizika kwa dakika 90 za mchezo na hatimaye Tanzanite kufuzu hatua inayo fuata kwa jumla ya idadi ya mabao 4-3.

Tanzanite imevunja kambi hii leo Disemba 21, 2021 ili wachezaji kuweza kurudi na kujiunga na timu zao za vilabu kwaajili ya maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu ya Wanawake (SWPL) inayotarajia kuanza kutimua vumbi Disemba 23, 2021 kisha kocha atakiita kikosi hicho mapema mwezi Januari kwaajili ya maandalizi ya mchezo wao wa hatua unaofuata, utakaowakutanisha na timu ya Etiopia mwezi Januari kati ya tarehe 21, 22, na 23, 2022.