KMKM Yakubali Yaishe Mbele ya Express
KIKOSI cha Express FC kutoka Uganda kimetinga kucheza hatua ya fainali ya michuano ya CECAFA Kagame Cup 2021 inayofanyika nchini Tanzania, baada ya kuwachapa KMKM bao 2-1 wapinzani wao hao kutoka visiwani Zanzibar kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza uliopigwa Agosti 10.
Mchezo huo uliochezwa majira ya saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam ulikuwa wa vuta ni kuvute kutokana na timu zote mbili kuhitaji kwenda katika hatua ya Fainali.
Timu ya KMKM ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuandika bao la kuongoza kupitia kwa mchezaji jezi namba (2) aitwae Ibrahim Abdallah Hamad; bao hilo likipatikana kwa njia ya faulo kunako dakika ya 45 kipindi cha kwanza, bao lilodumu mpka timu hizo zinakwenda kwenye mapumziko.
Kipindi cha pili timu zote ziliingia kwa kasi mpya, huku Express kutoka Uganda wakionekana kulisakama lango la KMKM mithili ya siafu na kunako dakika ya 56 kipindi hicho wakafanmikiwa kuandika bao kupitia mchezaji jezi namba 10, aitwae Muzamiru Mutyaba aliyekwenda kupiga mpira wa faulo uliojaa moja kwa moja kimyani na kusawazisha matokeo.
Mchezo huo ulikwenda sare mpaka dakika za mwisho ambapo timu ya Express ilifanikiwa kupata penati baada ya mchezaji wa KMKM kufanya madhambi kwenye eneo la hatari; penati hiyo ikipigwa na mchezaji jezi namba 7 Erick Kambale; aliyetumbukiza mpira huo nyavuni na kubadili ubao wa matokeo kunako dakika za lala salama.
Baada ya mchezo huo makocha wa timu zote mbili waliweza kuzungumza ambapo kocha wa KMKM Ali Vuai Shein alisema kuwa kikosi chake kimepambana kwa nguvu zote lakini makosa machache yaliyofanyika kipindi cha pili ndio yalipelekea wao kupoteza mchezo huo ambao walihitaji kushinda na kutinga hatua ya fainali.
Kocha huyo aliongeza kusema kuwa wachezaji wake wamecheza vizuri lakini wakati mwingine mpira huenda na bahati pia; hivyo, katika mchezo huo Express walifanikiwa kupata bahati ya kushinda licha ya kikosi chake cha KMKM kuonekana kuutawala mchezo katika vipindi vyote, hasa kwenye kipindi cha kwanza.
Kwa upande wa kocha Mkuu wa Express ya Uganda Wasswa Bossa, yeye alisema kuwa wachezaji wake walijitahidi kutumia nafasi walizozipata kutokana na kuwalazimisha KMKM wafanye makosa ambayo yaliweza kutoa fursa ya wao kupata magoli yote mawili licha ya kikosi hicho kuzidiwa katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo ambao ulionekana kutawaliwa na KMKM kutoka Zanzibar.
Mchezo wa nusu fainali ya pili utazikutanisha Azam FC dhidi ya Big Bullets kutoka Malawi, mchezo utakao pingwa siku ya juma tano 11 Agosti, 2021 kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi majira ya saa 1:00 usiku. Mshindi wa mchezo huo atakwenda kukutana na Express; huku walioshindwa wao wakitarajiwa kukutana kutafuta mshindi wa tatu pia.