Mafanikio Lukuki Sekta ya Michezo Ndani ya Mwaka
Imeelezwa hiyo Machi 16, 2022 Jijini Dodoma na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa alipokuwa akieleza mafanikio ya Wizara yake kwa kipindi cha mwaka mmoja madarakani mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mchengerwa alisema kuwa kutokana na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo sambamba na kutengwa kwa asilimia 5% ya fedha za Bahati Nasibu ndiko kumesaidia zaidi nchi kufikia maendeleo hayo,”Hadi kufikia Februali mwaka huu kiasi cha TZS Bilioni 1.55 kimepokelewa kutoka Hazina. Fedha hizi zimeanza kusaidia maendeleo mbalimbali ya michezo nchini na zitasaidia pia katika programu za uendelezaji wa miundombinu”.
Hata hivyo Mheshimiwa Mchengerwa aliweka wazi kuwa katika mwaka mmoja huu, serikali imekamilisha hatua muhinu za ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya michezo ikiwemo kukamilika kwa usanifu wa Uwanja wa soka wa Dodoma, kukamilika usanifu wa ujenzi wa viwanja vya mazoezi na kupumzikia wananchi vitakavyojengwa Dar es Salaam, Dodoma na Geita.
Hivi karibuni Waziri huyo alitembelea kikosi cha timu ya Taifa cha wasichana chini ya miaka 17 nchini Serengeti Girls, jina ambalo pia aliwabariki siku alipotembelea kambi yao huko visiwani Zanzibar huku akisema waende kuitangaza Serengeti Duniani kwani Serikali inamatarajio mengi na Imani kubwa kwa timu hiyo hasa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Timu ya Serengeti Girls kwa sasa ipo kwenye mbio za kuisaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia, michuano itakayo fanyika hapo baaye mwaka huu nchini India. Yote ikiwa ni mafanikio ya nchi kutoa timu zinazo shiriki mashindano makubwa ya kimataifa.
Tanzania pia ilipata bahati ya kuwa wenyeji wa Mashindano ya Soka kwa Walemavu Afrika (CANAF-2021) ambapo pamoja na kupokea takribani nchi 13 kutoka Afrika, Timu ya Taifa Tanzania ya soka la Walemavu Tembo Warriors ilikuwa miongoni mwa timu nne zilizofuzu kutoka Afrika kwenda Kombe la Dunia Uturuki Oktoba mwaka huu.