TFF Yaweka Wazi Uataratibu Kuelekea Ngao ya Jamii”
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa mwongozo wa utaratibu wa viingilio vya mchezo wa Ngao ya Jamii utakaowakutanisha watani wa jadi; Simba SC dhidi ya Young Africans unaotarajiwa kupigwa Septemba 25, 2021 majira ya saa 11:00 jioni kwenye dimba la Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Kuelekea maandalizi hayo TFF pamoja na Maofisa Habari wa timu hizo kongwe Tanzania na Afrika Mashariki walikutana Septemba, 21, 2021 na kuongea na waandishi wa habari za michezo ambapo ajenda kuu ilikuwa ni viwango vya viingilio ambavyo TFF imepanga kwa mashabiki watakao hudhuria kushuhudia mchezo huo, pamoja na maandalizi ya timu hizo kutoka kwa Maofisa Habari wa klabu hizo mbili.
Akitolea muongozo wa viingilio vya kwenye mchezo huo Ofisa Habari wa TFF Cliford Mario Ndimbo alisema kuwa bei itaanzia shilingi 30,000/= kwa VIP B; shilingi 20,000/= kwa waatazamaji wa VIP C; pamoja na wale wa viti vya rangi ya Machungwa huku viinglio kwa watazamaji wa viti vya rangi ya blue na kijani vikitajwa kuwa shilingi 10,000/=. Aliendelea kufafanua zaidi kuwa tiketi za VIP A hazitauzwa na badala yake nafasi hizo zitakauwa ni maalum kwa ajili ya watu an wageni ambao watakuwa na mualiko rasmi.
Ndimbo alitolea pia ufafanuzi swala zima la haki za matangazo ya mchezo huo kwa vyombo vya Habari na kusema kuwa TFF imekuwa na utaratibu mzuri wa utekelezaji wa mambo yake, hivyo kabla ya mchezo huo watawaalika tena wanahabari hao ili kuwaelezea jinsi ambavyo taratibu za urushaji wa matangazo ya mchezo huo zitakavyokuwa.
Naye Ofisa Habari wa Simba SC Ezekiel Kamwaga alisema kuwa timu imerejea kambini Septemba 21, 2021 kwa ajili ya kuendelea na maandalizi mara baada ya mapumziko ya siku mbili baada ya timu hiyo kutoka kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Dimba la Benjamini Mkapa dhidi ya TP Mazembe siku ya kilele cha ‘Simba Day’ (Septemba 19, 2021).
Kamwaga alieleza kuwa timu imejipanga vizuri si tu kwa mchezo huo bali pia kwa michezo mingine ya Ligi Kuu Soka Bara inayotarajiwa kuanza hivi karibuni mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu. Kamwaga aliwataka mashabiki wa Simba SC kuendelea kuiunga mkono timu yao kwa kuonesha umoja na ushirikiano kama ambavyo wamekuwa wakifanya hivyo wakati wakiazimisha wiki ya ‘Simba Day’.
Kwa upande wa timu ya Young Africans ambao wanatarajiwa kuwa wageni kwenye mchezo huo Ofisa Habari wa klabu hiyo Hassani Bumbuli alisema kuwa timu yao imewasili Septemba 20, 2021 kutoka Nchini Nigeria kwenye mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika uliowakutanisha na Rivers United Septemba 19, 2021.
Bumbuli aliweka bayana kuwa kwa upande wa timu yao walishajipanga kwa muda mrefu kwani ratiba ya mchezo huo ilikuwa inajulikana hivyo wachazaji wako tayari kuwakabili watani wao na kwamba timu ilifikia kambini kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mchezo huo.
Bumbuli aliwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo na kuwataka kufika kwa wingi kwenye mchezo huo wakiamini kupata matokeo mazuri huku akitoa angalizo kwa mashabiki kuwa kunauwezekano kikosi hicho kikawajumuisha wachezaji ambao mashabiki wamewakosa kwenye michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Rivers United.
Mchezo wa Ngao ya Jamii utapigwa ukiwa ndio wa ufunguzi kuelekea michezo mingine ya Ligi kuu Bara msimu 2021/2022 itakayoanza kutimua vumbi Septemba 27, 2021 kwa kupigwa michezo mitatu; Mtibwa Sugar dhidi ya Mbeya Kwanza kwenye Dimba la Jamhuri Mkoani Morogoro majira ya saa 8:00 mchana.
Michezo mingine; itakuwa ni kati ya Namungo na Geita Gold, mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Ilulu mkoani Lindi majira ya saa 10:00 jioni,huku mchezo wa mwisho kwa siku hiyo ukiwakutanisha Coastal Union ya Tanga dhidi ya Azam FC kwenye dimba la Mkwakwani mkoani Tanga mchezo utakao chezwa majira ya saa 10:00 jioni.