Rais Samia Kudhamini CECAFA Wanawake

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekubali ombi la kudhamini mashindano ya wanawake ya CECAFA baada ya kupokea maombi ya udhamini wa mashindano hayo yatakayo kuwa yakifanyika kila mwaka kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia ambaye pia ni Rais wa CECAFA.

Mhe. Rais Samia amekubali maombi hayo ya udhamini Agosti 22, 2021 alipokuwa akizungumza kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo pia zoezi la kukabidhiwa kombe na Timu ya Taifa U23 ambao ni  mabingwa wa mashindano ya CECAFA, mashindano yaliyo fanyika Nchini Ethiopia mwaka huu.

Mhe. Rais Samia aliongeza kuwa hapo awali Rais Karia alimfata na kumpa ombi la kumtaka kudhamnini mashindano hayo ya CECAFA CHAMPIONSHIP kwa wanawake kila mwaka huku akimpa mifano ya kumshawishi, hivyo mara baada ya kutafakari na kufanyia kazi na kuona umuhimu wa maombi hayo Rais Samia alikubali na kutamka rasmi kuwa yupo tayari sasa kudhamini michuano hiyo; na kwamba atafanya  namna atakavyoweza ili kufanikisha udhamini huo.

Aidha, Mhe. Rais ambaye pia amewahi kuwa mlezi wa timu za wanawake Tanzania wakati akiwa Makumu wa Rais kuwa serikali imeanzisha mfuko wa maendeleo ya michezo kwa lengo la kusaidia timu za Taifa nchini. Mfuko huo wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.5 kwa kuanza huku akisema kuwa kupitia vyanzo mbalimbali watahakikisha mfuko huo unazidi kutuna na hatimaye kuweza kukidhi mahitaji ya michezo nchini.

Hata hivyo, Rais Samia aliendelea kusema kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada ya kuweza kuondoa na kumaliza Tozo na ushuru mbalimbali kwa vifaa vya michezo hususani gharama kwenye nyasi bandia hiyo yote ni katika kuhakikisha wanaboresha muonekano wa viwanja nchini.

Mbali na hayo, yanayofanywa na serikali chini ya uongozi wa Rais Samia bado imekuwa ikiangalia pia jinsi ya kuweza kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana wadogo; kwani serikali imeanza kujenga kituo kwenye chuo cha Maendeleo ya  michezo Mkoani Mwanza.

Aliahidi pia kuendelea kujenga vituo vya kukuza na kuendeleza michezo kwa vijana wadogo vingi zaidi kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kulelea vipaji vya maendeleo ya michezo, halikadhalika serikali imepanga kujenga viwanja vitatu vya mazoezi kwenye maeneo mbalimbali nchini; lakini kwa awamu ya kwanza zoezi litaanzia na mikoa mitatu  ambayo ni; Dar es Salaam, Dodoma na Geita.

Ni kwa mara ya pili Mhe. Rais Samia anakutana na timu za Taifa zinazofanya vizuri kwenye mashindano ya mataifa yaliyo kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na kati, hapo awali kabla hajakalia kiti cha Urais alikutana na timu ya Taifa U17 mwaka 2017.