Rais Karia Afungua Kozi ya Ukocha wa Magolikipa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania limefungua mafunzo ya Ukocha wa Magolikipa inayotolewa na shirikisho la mpira wa miguu duniani (FIFA) inayotambulika kwa jina la (FIFA GOAL KEEPING COACHING COURSE) na kuipa nafasi Tanzania kuwapa mafunzo ya juu ya ukocha wa makipa kwa mara ya pili baada ya mafunzo ya aina hiyo kutolewa kwa mara ya kwanza mwaka 2016.
Makocha wa makipa wapato 26 kutoka timu za taifa na zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara (NBC Premier League) wamehudhuria kozi hiyo inayoongozwa na mkufunzi kutoka FIFA Aljandro Heredia ikiwa ni mwendelezo wa mafunzo yaliyopita yanayolenga kuwaongezea uwezo makocha wa magolikipa katika kutekeleza majukumu yao na kuongeza wigo mpana wa makocha wazawa kutumika katika timu za Taifa na vilabu mbalimbali ili kupunguza wimbi la utegemezi kutoka kwa makocha wa kigeni.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafuzo hayo Rais wa TFF Wallace Karia alianza kwa kuwapongeza washiriki wote kwa maamuzi sahihi ya kuhudhuria mafunzo hayo huku akifurahishwa na nyuso za wachezaji wengi wa zamani na kusema kuwa ni matamanio yake kuona wachezaji wa zamani wanashiriki katika kozi mbalimbali za mpira wa miguu ili kujihakikishia ajira baada ya kustaafu kucheza mpira.
Rais Karia hakuacha kugusia suala la makocha wa kigeni ambapo alisema ni wakati sasa umefika kwa makocha wazawa kujiamini na kuanza kuchangamkia fursa katika vilabu mbalmbali na hata historia inaonesha kwamba timu zilizofanya vizuri katika mashindano ya Afrika zote zina makocha wazawa, tatizo kubwa linalowakwamisha makocha wengi wazawa ni kutokujiamini na kutokupenda kujiendeleza katika Elimu.
Akaongeza kwa kusema kipindi ligi inaposimama ndio wakati sahihi wa kozi za ukocha kutolewa ili kutoa fursa kwa wachezaji na wengine wenye nia ya kujiendeleza kuhudhuria kuliko kwenda kufanya mambo mengine ambayo hayana manufaa katika tasnia yao.
Naye mkufunzi wa kozi hiyo Aljadro aliwaambia washiriki hao kwamba wana bahati ya kupata nafasi hii adhimu kushiriki kozi ya aina hiyo kwa mara ya pili; hivyo maarifa wanayoyapata TFF wakayatumie kwa manufaa yao. Alisema hivyo akilenga suala la ajira za ndani na nje lakini pia kwa manufaa ya Taifa ikiwa ni pamoja na kwenda kutumia mbinu walizozipata wakati wa mafunzo katika kuibua na kuvijenga vipaji vichanga kwa manufaa ya baadaye.
Akizunguza kwa niaba ya washiriki wenzake kocha wa magolikipa Ivo Mapunda alitoa ombi kwa Rais wa TFF akitaka makocha wa magolikipa waliopata mafunzo kupatiwa nafasi ya kufundisha katika vilabu au timu za Taifa. Alipendekeza kuwa ikiwezekana sheria ziwekwe kama ilivyo kwa makocha; kwamba ili mwalimu wa magolikipa aweze kukaa katika benchi la ufundi lazima awe amesoma na sio kuwekwa kwa kujuana ili kupunguza changamoto ya ajira kwa makocha waliosoma.
Washiriki 26 wamehudhuria mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na Josia S. Kasasi, Ally M. Mtinge, Steven J. Malashi, Adam A. Moshi, Mussa M. wanema, Shaban M. Dihile, Soud S Slim, Answile Asukile, Mansour A. Abdallah, Anna M. Joel, Eberhard E. Mhagama, Niwael K. Makuruta, Muharami M. Sultan, Salimu W. Tupa, Herry B. Menjady, Raphael D. Mpa, Fatuma O. Jawadu, Juma K. Juma, Agustine J. Malindi, Emmanuel S. Mwasile, Kibwana S. Nyogoli, Idd A. Mwinchumu, Ivo Mapunda, Hussein T. Katandula, Ally J. Shomari na Wilbert M. William.