Timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa Miaka 17 (Serengeti Girls) imewasili jijini Gaborone tarehe 7 Aprili 2026 kwa ajili ya mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 itakayochezwa tarehe 10 Aprili.
Mechi hiyo dhidi ya wenyeji Botswana itachezwa katika Uwanja wa Obeid Itani Chilume uliopo katika mji wa Francistown.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi cha Serengeti Girls, Kocha Mkuu Bakari Shime alisema timu imepata maandalizi ya kutosha ikiwemo mechi za kirafiki za kimataifa, hivyo matumaini ya kufanya vizuri ni makubwa.
Hiyo ni mechi ya kwanza kwa Serengeti Girls kuwania tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 na endapo itafanikiwa kuitoa Botswana hatua ya pili itacheza na Afrika Kusini.
Mara ya mwisho Serengeti Girls kufuzu Kombe la Dunia ilikuwa mwaka 2022 ikiifunga Cameroon ugenini mabao 4-1 katika Uwanja wa Ahmadou Ahidjo na nyumbani bao 1-0 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

