Young Africans Yaazimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi Kigumu

Mabingwa wa kihistoria nchini Dar Young Africans wamefanya utambulisho wa wachezaji wao wa msimu 2021/2022 katika siku ya kilele cha maazimisho ya wiki ya mwananchi huku Haji Sundey Manara akianza rasmi majukumu yake mbele ya kutambulisha kikosi hicho kipya mbele ya maelfu ya mashabiki waliofulika kushuduia tukio hilo.

Manara ametambulishwa rasmi na timu ya Young Africans Agosti 29, 2021 kwenye hafla ya kilele cha kuhitimisha wiki ya Wananchi (Young Africans) iliyofanyika kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, hafla iliyoambatana na mechi ya kujipima nguvu na timu ya Zanaco kutoka nchini Zambia.

Mchezo huo uliopigwa majira ya saa 1:00 usiku, uliandaliwa na timu ya Young Africans kwa lengo  maalum la kutaka kupima viwango vya sajili zao walizozifanya msimu huu; ili wabaini upungufu uliopo kwenye kikosi hicho ambacho kinasemekana kuwa ni bora.

Mchezo huo uliomalizika kwa timu ya Dar Young Africans kupoteza kwa kuruhusu mabao mawili kwa moja. Licha ya Young Africans kuanza kupata bao mnamo kipindi cha kwanza tu cha mchezo huo; bao lililofungwa na Heritier Makambo Jz(19) na  kusalia mpaka timu zinakwenda mapumziko.

Mambo yalibadilika kwa upande wao katika kipindi cha pili baada ya mwalimu Kelvin Kaindu kufanya mabadiliko kadhaa kwenye kikosi chake; mabadiliko ambayo kwa upande wa Zanaco yalikuwa chanya na tofauti ilivyokuwa kwa upande wa Young Africans. Young Africans wao walirudi kama wageni kwenye kipindi hicho baada ya kuvalia jezi yenye uzi wa rangi ya manjano ambayo kwa kawaida huashiria ugenini.

Ni mabadiliko ya Mchezaji Ackim (Jz-22) na John Sikaumbwe (Jz-25) ndio walioifungia timu yao Ya Zanaco mabao mawili ya ushindi; huku wote wakitokea benchi na kufanya mchezo huo wa kujaribu mitambo kwa klabu ya soka ya Dar es Salaam Young Africans kumalizika  kwa matokeo ya 2-1.

Afisa muhamasishaji wa klabu ya soka ya Young Africans Antonio Nugazi alisema kuwa lengo kubwa la kocha Nabi katika mchezo huo ilikuwa si kupata ushindi tu, bali ni kuangalia ama kutafuta jinsi ya kupanga kikosi chake cha kwanza na kuangalia makosa madogo madogo ili kuelewa jinsi ya kuyafanyia kazi makosa waliyoyabaini.

Hata hivyo, bado mabingwa hao wa kihistoria nchini wanayo nafasi ya kuongeza wachezaji wengine endapo wataona inafaa kufanya hivyo ili kurekebisha makosa waliyo yabaini kupitia mchezo huo wa kirafiki.

Mgeni rasmi kwenye sherehe hizo alikuwa ni makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah, huku wageni wengine wa heshima wakiwa ni Waziri wa Habari,Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia, Mbunge wa Wilaya ya Kinondoni Abbas Tarimba, Mwenyekiti wa klabu ya Young Africans Dr Mshindo Msola, Eng. Hersi Said na wengine wengi.

Wachezaji waliotambulishwa kwa upande wa timu ya Young Africans ni; Djigui Diarra (GK), Ramadhani Kabwili(GK), Erick Johola(GK), Djuma Shabani, Kibwana Shomari, Adeyum Swaleh, Yassin Mustafa, Dickson Job, Bakari Nondo Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Deus David Kaseke, Feisal Salum (Fei Toto), Zawadi Mauya, Said Ntibazonkiza, Ditram Nchimbi, Farid Mussa, Balama Mapinduzi, Dickson Ambundo, Fiston Mayele, Heritier Makambo, Yacouba Songne, Yusufu Athumani, Jesus Moloko, Paul Godfrey na Khalid Aucho.

Dar Young Africans sasa wanaangazia mchezo wa Klabu Bingwa Afrika utakao wakutanisha na timu ya Rivers United kutokea nchini Nigeria ikiwa ni moja kati ya timu mbili kutoka nchini Tanzania zinazoshiriki kwenye mashindano hayo, timu nyingine ikiwa ni ya Simba Sports Club ambao wao wataazimisha siku yao mwezi Septemba mwaka huu.