Mchezo wa fainali za Kombe la Mapinduzi uliowakutanisha Young Africans na Simba ulimalizika kwa timu ya Young Africans kutwaa Kombe hilo ambalo lilikuwa likichukuliwa mara kadhaa na timu ya Simba, Azam; na Mtibwa Sugar ambayo ililichukua mwaka 2020 ikiwatoa Simba.
Mtanange huo uliopigwa Januari 13, 2021 kwenye uwanja wa Amani, ulikusanya mashabiki lukuki na ulikuwa wa kukata na shoka kutokana na timu zilizokutana katika hatua hiyo ya fainali ambazo zote zilitoka Dar es Salaam, Kariakoo; timu ambazo kihistoria zinapokutana huwa na upinzani mkubwa kutokana na utani wao wa jadi. Fainali hiyo ilikuwa kali na yenye mvuto wa kipekee hapo Mjini Zanzibar ambapo umati wa mashabiki ulifulika na kuwafanya baadhi yao kukosa nafasi ya kukaa.
Kipindi cha kwanza cha mchezo huo kilianza kwa kasi wakati huo timu zote zilikuwa makini ili kuhakikisha kuwa haziruhusu bao la mapema. Young Africans walionekana kuwa bora zaidi katika dakika za awali kabla Simba hawajachangamka na kuanza kuutawala mpira.
Kila timu ilikuwa ikifanya mashambulizi kwa kuvizia huku ikijilinda kwa umakini zaidi kutokana na umuhimu wa mchezo huo. Kulikuwa na kosa kosa za hapa na pale lakini zote hazikuzaa matunda mpaka kipindi cha kwanza kinaisha si Simba wala Young Africans iliyoweza kuliona lango la mwenziwe.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ile ile huku Simba ikionesha uchu wa kulitwaa kombe hilo kutokana na kulikosa kosa mara nyingi licha ya kufanikiwa kutinga fainali kama mwaka 2020; kwani ilicheza fainali kama ilivyokuwa awamu hii, hivyo ilizidisha mashambulizi zaidi katika lango la Young Africans. Pamoja na juhudi hizo bado dakika 90 zilikamilika pasipo nyavu kutikiswa na hivyo kupelekea mchezo huo kuamuriwa kwa njia ya mikwaju ya penati ambapo Young Africans ilipata penati 4 huku Simba ikiambulia 3. Penati ya Said Ntibazonkiza ndiyo iliyomaliza mchezo na kuwapa Young Africans taji hilo mabalo ililikosa kwa muda mrefu kidogo.
Kwa matokeo hayo Young Africans ikawa imefanikiwa kuanza kuirudisha heshma ya kuchukua vikombe kama kocha wake Cedric Kaze alivyoongea wakati akihojiwa na waadishi wa habari mara baada ya kuvuka hatua ya nusu fainali. Kocha Kaze alisema kuwa kila mechi kwake ni fainali na kila kikombe ni muhimu kwake. Hivyo yeye amekuja kurejesha furaha na heshma ya kutwaa vikombe kwani anajua ukubwa wa timu hiyo yenye mashabiki wengi ndani na nje ya nchi.
Akizungumza baada ya mchezo huo kocha Mkuu wa kikosi cha Young Africans Cedric Kaze aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kuhakikisha wanatimiza malengo ya klabu yao ikiwa ni pamoja na maelekezo yake ya kutwaa kila kikombe kinachojitokeza mbele yao. Hata hivyo, aliwapongeza wachezaji wa Simba pia kwa kuonesha upinzani kwani haikuwa rahisi kutwaa kikombe mbele ya mabingwa hao watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara.
Naye kocha wa Simba Selemani Matola alisema kuwa kikosi chake kimepambana kadri kilivyoweza kikafanikiwa kutengeneza nafasi nyingi lakini haikuwa bahati yao. Aliongeza kwa kuipongeza timu ya Young Africans kwa kutwaa ubingwa huo ambao mwaka jana ulitwaliwa na Mtibwa Sukari yenye makazi yake Mjini Morogoro; na akasema kuwa mpira ndivyo hivyo ulivyo.
Wachezaji walionza kwa upande wa wenyeji Young Africans ni Farouk Shikalo GK, Kibwana Shomari, Adeyum Salehe/Paul Gofrey, Juma Makapu, Abdallah Shaibu, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Zawadi Mauya, Haruna Niyonzima ©, Michael Sarpong /Waziri Journior na Said Ntibanzokiza (ANTIBIOTIC). Huku kwa upande wa Simba wakiwa: Beno Kakolanya GK, David Kameta, Gadiel Michael, Kenedy Juma, Joash Onyango, Tandeo Lwanga, Hassan Dilunga/Chris Mugalu, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere,Francis Kahata na Miraji Athumani/ Ibrahim Ajib(Kadabla).
Fainali hizo zilihudhuriwa na Mh. Rais wa Serikali ya Awamu ya Nane na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Daktari Hussein Mwinyi, Makamu wa kwanza wa Rais Seif Hamad Sharifu, Makamu wa Pili wa Rais Mh.Hemed Suleman, Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Zanzibar Mh. Tabia Mwita, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia na makamu wake wote (Athumani Nyamlani1na Steven Mnguto 2), Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania, Alimas Kasongo; Rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar, Seif Pandu (Seif Boss) Makamu wake Salum Ubwa na viongozi mbalimbali wengi wa soka, serikali, wadhamini na wadau wengine mpira wa miguu kwa ujumla.
Tuzo ya mchezaji Bora wa fainali hizo ilikwenda kwa Francis Kahata akijinyakulia kitita cha shilingi milioni nne (4,000,000/=), Tuzo ya Mfungaji bora ilikwenda kwa Miraji Athumani, akipata shilingi Milioni tatu (3, 000,000/=) huku Mchezaji Bora wa mechi hiyo ya fainali akiwa Joash Onyango aliyepata milioni moja (1,000,000/=) wachezaji wote wakiwa ni kutoka Klabu ya Simba (“Simba Sports Club”)
Young Africans wamefanikiwa kuchukua ubingwa wa Kombe la Mapinduzi huku wakiwa wanaongoza Ligii Kuu Bara pasipokupoteza hata mchezo mmoja; huku wenzao Simba wakiwa nafasi ya pili baada ya kupoteza michezo miwili na kutoka sare katika mchezo mmoja.