Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatupa karata yake ya mwisho Desemba 30, 2025 dhidi ya Tunisia katika mechi ya hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika (AFCON).

    Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Olympic, Rabat, Morocco kuanzia saa moja kamili usiku.

    Akizungumzia mechi hiyo ya Kundi C, Kocha Mkuu wa Stars, Miguel Gamondi ambaye ni raia wa Argentina alisema:

    “Ni mechi muhimu kwetu na tunacheza na Tunisia ambao wametoka kupoteza mechi, hivyo watakuja kwa nguvu zaidi kujaribu kupata matokeo, lakini tuko tayari kupambana.

    “Nina wachezaji wengi wanaotamani kuliwakilisha Taifa vizuri, na hii ni nafasi yetu ya mwisho”.

    Naye kiungo wa Stars, Novatus Dismas alisema: “Tumejiandaa vizuri kwa mechi, tunaamini itakuwa ngumu kwa sababu Tunisia ni timu kubwa.

    “Tunahitaji matokeo ya ushindi ili kufuzu hatua ya mtoano ambayo ni malengo yetu kama timu, tuna imani tutaweka historia mpya.”

    Tanzania inashikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi lake ikiwa na pointi moja baada ya kupoteza dhidi ya Nigeria na kutoka sare na Uganda, wakati Tunisia iko nafasi ya pili na pointi tatu baada ya kupoteza dhidi ya Nigeria na kushinda dhidi ya Uganda.

    Share.