HISTORIA YA MPIRA WA MIGUU WA MASHINANI (GRASSROOTS FOOTBALL)
FIFA ilitambulisha Mpira wa miguu wa mashinani mwaka 2009 mara baada ya kukamilika kwa utafiti kuhusu jinsi ya kuwasimamia, kuwaongoza na kuwapa fursa ya kucheza mpira wa miguu wavulana na wasichana, utafiti huo ulifanyika katika kisiwa cha Maurititus ambapo FIFA iliendesha mafunzo kwa walimu wa shule za msingi katika Kisiwa hicho na baada ya mafunzo mkakati wa ufundishaji ukaanza rasmi shuleni.
Mwaka 2011 mwezi Desemba FIFA iliendesha kozi nchini Tanzania ya FIFA Grassroots Football Coaching Course kwa muda wa siku tano na walimu wapatao 26 waliweza kushiriki katika mafunzo hayo, walimu hao walitoka katika wilaya tatu zilizokuwepo wakati huo katika mkoa wa Dar es salaam, ambazo ni Ilala, Temeke na Kinondoni, wilaya ya Ilala ilitoa walimu 12, Kinondoni 08 na Temeke 04.
Walimu hao walitoka katika shule zifuatazo, Ally H Mwinyi, Karume, Dr Omary A Juma, Bunju A, Mwananyamala B, Mwongozo, Hekima na Makumbusho kutoka Wilaya ya Kinondoni, Wilaya ya Ilala shule zilikuwa ni, Boma, Uhuru-Mchanganyiko, Msimbazi, Airwing, Mwangaza, Chanika, Buguruni Kisiwani, Tabata, Kinyerezi, Kiwalani, Kigogo Fresh na Uhuru Wasichana.Wilaya ya Temeke shule zilikuwa ni Mbagala kuu, Mtoni Kijichi, Kingugi na Mtoni Kwa Azizi Ally.Shule zote hizo ni za serikali.
FIFA iliwakabidhi vyeti vya ushiriki wa kozi hiyo, jukumu kubwa la walimu hao lilikuwa ni kurudi shuleni na kwenda kufundisha watoto yaani wavulana na wasichana kuanzia umri wa miaka 04 hadi 12. Lengo kuu la FIFA/TFF ni kuongeza washiriki katika uchezaji wa mpira wa miguu shuleni kwa watoto wa jinsi zote chini ya usimamizi wa walimu ambao wanataaluma ya kusimamia, kuongoza na kutoa fursa ya uchezaji wa mpira wa miguu kwa njia ya uhamasishaji, hivyo FIFA iliutambulisha rasmi mpira wa miguu wa mashinani
Nchini Tanzania.
FALSAFA YA MPIRA WA MIGUU WA MASHINANI:
Falsafa FIFA Grassroots ni muongozo unaomwelekeza kocha mambo gani anayotakiwa kufanya akiwa anafanya kazi ya kusimamia, kuongoza, kutoa fursa ya kucheza mpira wa miguu kwa wavulana na wasichana kwa kutumia njia ya uhamasishaji.
Falsafa ya FIFA Grassroots imejikita kwa watoto kuanzia umri wa miaka 04 hadi miaka 12, ikumbukwe kwamba watoto wenye umri huu bado wapo shuleni wakiwa wanaendelea na masomo katika shule wasomazo. Falsafa inaeleza kwamba ili yafanyike haya ni vema anayetaka kufanya kazi ya kuwasimamia, kuwaongoza watoto na kuwapa fursa ya kucheza mpira wa miguu ni lazima awe amepata elimu ili aweze kuifanya kazi yake kwa ukamilifu.
Falsafa inaamini kwamba watoto ni rahisi kuingia katika mfumo wa mafunzo kwani sehemu kubwa ya Maisha ya kawaida ya watoto yanatawaliwa na michezo ikiwemo mpira wa miguu. Lakini usitarajie watoto ulionao katika mafunzo wote wanaweza kuja kuwa na kiwango cha juu cha uchezaji, wakati mwingine mpira wa miguu wa mashinani unatafsiriwa kama ni shughuli ziletazo burdani.
Hivyo kabla ya kuanza utaratibu wa ufundishaji ni jambo la msingi kuyafanya yafuatayo, kujitambulisha katika mamlaka zilizopo hapo, mamlaka hizo zaweza kuwa Kijiji, Kitongoji, Kata, Tarafa, Wilaya au Mkoa.Kupitia mamlaka hizo itakuwa rahisi kwa mwalimu kufanya kazi zako vizuri kwani utakuwa unatambulika. Unapaswa kuyaelewa mazingira ulipo na kuendana na tamaduni zilizopo hapo unapotarajia kuendesha mafunzo ya mpira wa miguu wa mashinani.
Falsafa inasisitiza mazoezi magumu, mbinu ngumu unashauriwa mwalimu usiyafanye hayo. Falsafa inaamini kwamba kucheza ni njia bora katika ujifunzaji, mpira wa miguu wa mashinani husaidia kudumisha mahusiano mema, kuimarisha hali za kitimu na kuongeza furaha kwa watoto. Falsafa inasisitiza ni jambo la msingi sana kuwa na mahusiano mazuri na wazazi, jamii, viongozi wa dini na viongozi wa mamlaka zilizotajwa hapo awali.
Falsafa ya mpira wa miguu wa mashinani inaelezea mwalimu wa watoto ni lazima awe na nguvu yenye mtiririko wa kubadilikabadilika, mwenye shauku la kutaka kufanya mambo mazuri kwa watoto, awe tayari kuwamotisha watoto, ukiwa na watoto usifanye vitu vikawa vigumu, anza katika hali rahisi kwenda katika ugumu.
Mpira wa miguu wa mashinani hauhitaji miundo mbinu mikubwa, bali inahitaji eneo lililo salama halina vitu hatarishi kama vile vipande vya chupa, mawe, misumari, hivyo mwalimu anajukumu la kuhakikisha kabla ya kuwaalika watoto kucheza yampasa kukagua eneo husika kikamilifu. Lakini mpira wa miguu wa mitaani ni sehemu pia ya shughuli za mpira wa miguu wa mashinani hasa wakati wa tamasha, pia soka la ufukweni na soka la ndani(futsal) kwa pamoja ni shemu ya mpira wa miguu wa mashinani.
Mwalimu ambaye tayari ameshapata mafunzo ya awali ya kufundisha mpira wa miguu anapaswa kutambua kwamba anao wajibu wa kusaidia kikamilifu uchezwaji wa michezo hiyo.
Yote kwa yote, Falsafa ya mpira wa miguu wa mashinani ni mwongozo sahihi ili kuweza kwenda sambamba na mtaala wa ufundishaji wa mpira wa miguu kuanzia ngazi hii ya awali,” Ieleweke kwamba mtoto anayecheza mpira sasa ni mchezaji wa keshokutwa na kijana anayecheza mpira wa miguu sasa ndiye mchezaji wa kesho”. Hivyo unahitajika msingi madhubuti katika ufundishaji wa mpira wa miguu ili tuweze kuwa na timu za vilabu nzuri na timu za taifa zilizo imara.
MAJUKUMU YA MWALIMU:
- Kusisitiza hali zote za uchezaji na kupanga mechi nyingi ndogo ndogo.
- Kutumia shughuli katika kuelekeza na kufundisha watoto (yaani mchezo na mazoezi ya kiufundi).
- Kutoa maelekezo kuwiana na uwezo walio nao watoto.
- Kuwaongoza watoto na kuwa mfano kwao.
- Kuwasaidia kukua wawe wanaume au wanawake.
- Kuyabaini na kuyachukua yote kama majukumu yako.
- Una jukumu la kuhakikisha usalama na huduma ya kwanza kwa watoto.
MALENGO YA MWALIMU:
- Kufurahi kucheza na watoto.
- Kutaka kuwajua watoto kwa undani Zaidi.
- Kuwa mfano au kioo kwa watoto.
- Kuandaa mambo katika ubora lakini uvumilivu ni jambo muhimu.
- Kuwasikiliza watoto.
- Kuwa na mawasiliano thabiti.
- Kubaini hali ya kujiamini ya watoto na kulidhihirisha hilo.
TABIA AMBAZO HATAKIWI KUWA NAZO MWALIMU:
- Kufoka au kuhamaki, kuchukia unapokuwa na watoto.
- Kuwasimamia, kuwaongoza, kuwauliza au kuwataka wacheze kama watu wazima.
- Kusahau motisha kubwa ya watoto ni kucheza mpira wa miguu.
- Kutoa maelezo marefu pasipo kuwapa mpira wacheze.
- Kila mara unaingilia mchezo.
- Kujikita katika matokeo pasipo kuangalia hali ya mchezo.
- Kumsema au kumsimanga mchezaji mbele ya wenzake afanyapo tofauti na utakavyo
USHIRIKISHWAJI WA WATOTO WA KIUME NA WA KIKE KATIKA UCHEZAJI WA MPIRA WA MIGUU:
Kwa miaka mingi iliyopita mataifa mengi yalikuwa hayaruhusu watoto wa jinsi tofauti kucheza mpira wa miguu pamoja hii ni kutokana na sababu za kiutamaduni. Wasichana waliweza kuruhusiwa kucheza na wasichana wenzao.
Katika elimu mataifa mengi sasa yameanzisha mfumo wa elimu ya mchanganyiko wa jinsi (wavulana na wasichana), hali hii imepelekea sasa wavulana na wasichana kuanza kucheza mpira wa miguu pamoja katika mfumo usio rasmi. Hatua endelevu za uchezaji wa mpira wa miguu kwa wavulana na wasichana haitofautiani kwani wote wanahitaji kupatiwa ufundi, uwezo wa kuusoma mchezo na mawasiliano.
Mataifa yaliyoendelea hasa Ulaya na Amerika wao wanawashirikisha wavulana na wasichana kuanzia umri wa miaka 04 hadi miaka 19, lakini kwa mataifa ya Afrika wavulana na wasichana wanashiriki katika kucheza mpira wa miguu kuanzia umri wa miaka 04 hadi miaka 12, ambapo hutenganishwa na kuanza kuendelezwa wakiwa jinsi moja kuanzia miaka 13 na kuendelea.
Kucheza pamoja kati ya wavulana na wasichana kuna faida za msingi zifuatazo, kuleta usawa katika jinsi zote, kuondoa hofu na kujenga hali ya kusaidiana na kushirikiana, kuboresha mahusiano miongoni mwao, kuheshimiana, pia hujenga taswira chanya kwamba wasichana wanaweza kujifunza kucheza mpira wa miguu na kuwa wachezaji wakubwa hapo baadae, wasichana hujenga hali ya kujiamini, vile vile uwezo na umakini huimarika zaidi wanapokuwa wanacheza.
Yote kwa yote uchezaji wa mpira wa miguu kwa jinsi zote huleta misingi mizuri katika jamii zetu kwa kuondoa hali ya unyanyapaa na ubaguzi kijinsi, kuimarisha na kusaidia ustawi wa jamii kwa kuweza kuinua hali zao za kiuchumi.
BAADHI YA MAJUKUMU YA KUZINGATIA KATIKA KUZUIA AJALI MCHEZONI AU MAZOEZINI.
·
MAZINGIRA
YAWE SALAMA:
Eneo hili linajumuisha
yafuatayo, hali ya hewa ya siku hiyo (yaweza kuwa na upepo mkali, mvua kubwa
zinazoambatana na radi, Jua kali linaloambatana na joto kali, Baridi kali), Mwalimu
kabla ya kuwaalika watoto uwanjani lazima ajiridhishe na hali ya hewa ya siku hiyo
kwa kuangalia vielelezo hivyo. Eneo jingine
analopaswa kuliangalia ni eneo la kuchezea, uwanja ni salama kwa watoto
kucheza? Kama kuna vitu hatarishi kama vile vipande vya chupa, mawe, miba, misumari
nk, anapaswa kuviondoa vitu hivyo kabla hajapanga kiwanja cha mchezo. Pasiwe na muingiliano wa watembeao kwa miguu, waendesha
baiskeli, pikipiki au magari.
PANGA KAZI ZAKO:
Mwalimu anatakiwa ajue katika ufanyaji wa kazi zake awe anajua anapaswa kuanza na nini na kumaliza na nini.
KAGUA WACHEZAJI KABLA HAWAJAANZA KUCHEZA:
Mwalimu unapaswa kuwakagua watoto/wachezaji kabla ya kuwaalika uwanjani ili kama kuna mtoto ambaye ana majeraha aweze kupatiwa huduma ya kwanza na kama jeraha lake ni kubwa kiasi ambacho hawezi kucheza siku hiyo. Mwalimu anapaswa kutumia busara na hekima ili kumshawishi mtoto ili apatiwe tiba.
UMRI WA WACHEZAJI:
Mwalimu anapaswa kuzingatia umri wa watoto/wachezaji siyo vizuri kuwachanganya watoto kiumri ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea, mfano: watoto wa umri wa miaka 6 unawachanganya na watoto wenye umri wa miaka 12 (usifanye hivyo).
ULINZI NA USALAMA KWA WATOTO:
Ulinzi ni mbinu, hatua, au hali ya kuweka mtu au kitu katika mfumo salama dhidi ya madhara ambayo yangemtokea. Usalama ni hali ya kutokuwa na hatari hofu, vurugu au madhara kwa mtu, mali au jamii kwa ujumla.
Mwalimu ana jukumu la kuhakikisha watoto muda wote anapokuwa nao wanalindwa na kuwa salama, kabla ya mazoezi, wakati wakiwa wanacheza na baada ya kumaliza mazoezi au mchezo. Kuyatekeleza haya mwalimu na wasaidizi wake wanapaswa kufika kabla ya watoto hawajafika na kuandaa eneo la
MFUMO WA UFUNDISHAJI WA MPIRA WA MIGUU WA MASHINANI:
Mfumo wa ufundishaji wa mpira wa miguu wa mashinani, unafanyika kwa kuyatafsiri kivitendo maeneo makuu matano yafuatayo:
· Kupasha mwili joto.
· Mchezo wa kwanza.
· Mazoezi ya kiufundi.
· Mchezo wa pili.
· Kupoza mwili joto.
Mfumo wa ufundishaji humsaidia mwalimu kwenda sambamba na kile alichukikusudia kukifundisha kwa watoto/wachezaji hivyo ni jambo la msingi mwalimu kuwa na mpango wenye mtiririko wa ufundishaji.
Katika kuna hatua za ufundishaji kuna vipengele hivi vifuatavyo, shughuli, mpango na ayazingatiayo kocha, kunakuwa na tathimini ya wachezaji, tathimini ya kocha, maoni na mapendekezo ili kuboresha ufundishaji, kisha lazima kocha aandike jina lake na kuweka saini yake pamoja na kuandika tarehe ya siku aliyofundisha kipindi chake.
MPIRA WA MIGUU SHULENI (FIFA FOOTBALL FOR SCHOOL):
Utangulizi:
Mpira wa miguu shuleni ulitambulishwa na FIFA mwaka 2009 na ilipofika Aprili 2024 mpango huu ulitambulishwa rasmi na FIFA hapa Tanzania ambapo FIFA iliendesha kozi ya siku 4 kwa walimu wa michezo toka shule mbali mbali nchini.
Jumla ya walimu wa sekondari na wa msingi wapatao 46 waliweza kushiriki katika mafunzo hayo na siku ya nne walihitimisha mafunzo hayo kwa kushiriki katika tamasha la FIFA FOOTBALL FOR SCHOOLS lililoshirikisha wanafunzi wapato 96 kutoka shule ya msingi ya Fountain Gate Academy, tamasha lilifanyika katika uwanja wa Benjamini Mkapa.
Siku hiyo ndipo FOOTBALL FOR SCHOOLS ilizinduliwa rasmi na zoezi la uzinduzi lilifanywa na Mh, Gerson Msigwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.Katika nasaha zake kwanza aliipongeza FIFA na TFF kwa kuhakikisha uwezeshaji wa kozi mbali mbali unafanyanyika kulingana na mahitaji, akamaliza kwa kuwasihi washiriki wote wa mafunzo hayo waende wakafundishe kama walivyofundishwa.
Mpira wa miguu shuleni ni utaratibu wa ufundishaji wa mpira wa miguu na stadi za maisha, ufundishaji huu umegawanyika katika makundi yafuatayo kiumri, miaka 4 – 7, miaka 8 – 11 na miaka 12 -14, mpira wa miguu shuleni ni sehemu wa mpira wa miguu wa mashinani hapa mwalimu anapata mwendelezo wa nini cha kufanya kutokana na umri wa watoto/wachezaji alionao.
FIFA mwishoni mwa mafunzo hayo ilikabidhi vyeti vya ushiriki wa Mpira wa miguu shuleni pamoja na nukuu za kufundishia kulingana na umri walionao watoto/wachezaji, ambapo kila mshiriki aliweza kupokea nukuu hizo kupitia app maalum ya FIFA ambapo kila mshiriki aliitafuta kupitia katika simu yake.
HITIMISHO:
TFF inawezesha mafunzo haya na Grassroots Football coaching course ambayo ndio mafunzo ya awali ya ualimu wa mpira wa miguu.TFF inawasihi kwa yeyote anayehitaji kushiriki katika mafunzo ya ualimu wa mpira wa miguu afanye mawasiliano na Idara ya Ufundi ya TFF ili upate maelekezo ya kutosha.
