Timu ya vijana ya U15 kuendeleza vipaji (TDS) baada ya kukamilisha maandalizi yake ya muda mrefu, sasa ipo tayari kutetea ubingwa wake kwa mara ya 3 mfululizo katika michuano ya CAF ya African School Football Championship (ASFC) jijini Harare, Zimbabwe.

    TDS imetoka kucheza mashindano ya Soccer School yaliyofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa Machi na kuishia hatua ya nusu fainali, ikiondolewa na TDS U17 kwa mikwaju ya penalti.

    Akizungumzia maandalizi yao Kocha Mkuu, Boniface Pawasa amesema kikosi chake kina utayari wa hali ya juu kuhakikisha kinatetea ubingwa.

    Alisema anatarajia ushindani mkubwa mwaka huu kulingana na timu ambazo zimefuzu, huku akizitaja Morocco, Zambia na Senegal kuwa ndio zaidi zitaongeza ushindani kulingana na ubora wao.

    “Tumekuwa tukizifuatilia timu pinzani kwa kuangalia baadhi ya mechi zao, hivyo naamini kupitia mafunzo tuliyoyafanya kwa kipindi chote hadi kufikia muda wa mechi zetu tutakuwa tayari kupata matokea mbele yao,” alisema Pawasa.

    Ameushukuru uongozi wa TFF chini ya Rais Wallace Karia kwa kuiwezesha timu hiyo kupata mahitaji yake yote kwa wakati, pamoja na ushirikiano mkubwa kutoka kwa Sekretarieti ya TFF.

    Pawasa amewataka Watanzania kuwa na Imani kubwa na vijana hao, akisisitiza wasichoke kuwaombea pamoja na kusimama nao kwa nyakati zote.

    Timu hiyo inatarajia kuondoka tarehe 2 Aprili, na itatupa karata yake ya kwanza kwenye mashindano hayo tarehe 4 Aprili.

    Share.