Timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 17 (Serengeti Girls) imewasili nchini Tunisia kuendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi ya kwanza ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Botswana itakayochezwa Aprili 10, 2026.

    Ikiwa nchini Tunisia, Serengeti Girls itacheza mechi mbili za kirafiki na timu ya Taifa ya Tunisia Machi 29 na Aprili 4 2026 katika mji wa Monastir.

    Akizungumzia maandalizi ya mechi hizo, Kocha Mkuu wa Serengeti Girls, Bakari Shime alisema mechi hizo ni muhimu kwa kikosi chake kwa sababu wachezaji wengi ni wapya na hawana uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa.

    “Ni mechi zitakazotupa taswira ya timu kuelekea mechi dhidi ya Botswana. Naamini hiki ni kipimo sahihi na wachezaji watafanya vizuri na kupata matokeo,” alisema Shime.

    Wachezaji 22 waliojumuishwa katika kikosi hicho cha Serengeti Girls ni Nusrat Jafari (Fountain Gate Princess), Robby Ngeye (Alliance Girls), Aneth Masala (JKT Queens), Devotha Isack (JKT Queens), Bhoke Magere (Mashujaa Queens), Odilia France (JKT Queens), Neema Mtunzi (Simba Queens), Elizabeth Chenge (JKT Queens), Anna Koku (Mwanga City) na Christer Basil wa klabu ya JKT Queens.

    Wengine ni Fatuma Khamis (Tausi FC), Yasinta Michael (Yanga Princess), Neema Thomas (JKT Queens), Harrier Juma (Yanga Princess), Bahati Steven (Bunda Queens), Helena Mtundagi (Fountain Gate Princess), Asha Ramadhani (Simba Queens), Norah Mushi (JKT Queens), Bahati Goma (JKT Queens), Janeth Matulanga (JKT Queens), Sundy Masasila (JKT Queens) na Eva Charles (Ilala Queens).

    Share.