Ni ‘derby’ ya Simba Queens, Yanga Princess TWPL
Ni mechi namba 96 ya Ligi Kuu ya Wanawake
Tanzania (TWPL) kati ya Simba Queens na Yanga Princess itakayochezwa tarehe 15 Mei 2026 Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Akizungumza mechi hiyo itakayoanza saa 11 kamili jioni, Kocha msaidizi wa Yanga Princess, Said Maulid alisema matayarisho yao yamekamilika.
“Tumewafuatilia wapinzani wetu katika baadhi ya mechi, hivyo tumejipanga kwenda kutumia udhaifu wao kupata ushindi,” alisema.
Naye mchezaji mwandamizi wa timu hiyo Maimuna Kaimu alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo, kwani azma yao ni kutwaa ubingwa.
“Mechi ya kesho (leo) itatupatia mwanga katika mbio za ubingwa msimu huu. Hatutaki kupoteza tena mbele ya Simba Queens,” alisema Kaimu .
Kwa upande wa Kocha mwenyeji Musa Mgosi alisema wamejipanga vyema kuhakikisha wanapata ushindi mwingine mbele ya wapinzani na watani zao wa jadi.
“Maandalizi yetu ni kwa ajili ya kuhakikisha tunakwenda kushinda ili tubebe ubingwa,”alisema Mgosi.
Nahodha wa Queens, Aisha Mnunka alisema kwenye swala la ufundi walimu wameshafanyia kazi kwa asilimia kubwa uwanja wa mazoezi, hivyo kilichobaki ni wao kwenda kufanyia kazi Azam Complex.

