Tanzanite yajinoa Z’bar, ikiisubiri Cameroo

    Ikiwa zimesalia siku tatu kabla  ya timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 (Tanzanite) kuvaana na Cameroon katika mechi ya marudiano kufuzu Kombe la Dunia, timu hiyo imeendelea na mazoezi makali kuhakikisha inapata ushindi.

    Tanzanite imepiga kambi Zanzibar mara baada ya kurejea nchini tarehe 4 Mei 2026 ikitokea Cameroon kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ambapo ilipoteza kwa mabao 3-1.

    Timu hiyo inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ili irate tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Poland mwezi Septemba mwaka huu.

    Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Tanzanite, Bakari Shime alisema:

    “Mpaka sasa timu ina asilimia zaidi ya 80 ya kufuzu Kombe la Dunia kutokana na maandalizi yaliyofanyika na ubora wa kikosi changu.”

    Shime aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi siku ya mechi ili kuwapa hamasa wachezaji na kuonesha uzalendo kwa taifa lao.

    Mechi ya marudiano kati ya Tanzania na Cameroon itachezwa tarehe 10 Mei katika Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

    Share.