Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imeibuka mshindi wa tatu katika Kundi B la michuano ya FIFA Series 2026 iliyochezwa Kigali, Rwanda.
Stars imeshika nafasi hiyo baada ya kuifunga Macau mabao 6-0 katika Uwanja wa Kigali Pele tarehe 29 Machi 2026.
Bao la mapema la Stars lilipatikana baada ya mchezaji wa Macau, Amancio Manuel kujifunga dakika ya 16, huku mabao mengine yakifungwa na Bakari Mwamnyeto, Mudathir Yahaya, Paul Peter, Novatus Dismas na Tarryn Allarakhia.
Baada ya ushindi huo, Kocha Mkuu wa Stars l, Miguel Gamondi alisema:
“Tuna hisia mseto ya ushindi huu, tunafurahi tumeshinda mchezo wa pili kwa mabao mengi lakini kiukweli hatuna furaha sana kwa sababu tulipoteza mechi ya kwanza ambayo tulipaswa kushinda”.
Timu ya Aruba imeibuka bingwa wa kundi B baada ya kuifunga Liechtenstein mabao 4-1. Kundi hilo lilijumuisha timu za Tanzania, Macau, Aruba na Liechtenstein.
Kwa upande mwingine, timu ya taifa ya Kenya (Harambee Stars) waliokua kundi A wamemaliza katika nafasi ya tatu baada ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya Grenada huku ubingwa wa kundi hilo ukibebwa na timu mwenyeji Rwanda baada ya kuifunga Estonia mabao 2-0.
Lengo la kuanzishwa michuano hii ya FIFA Series ni kutoa nafasi kwa timu za taifa kutoka mabara tofauti hasa timu zilizo chini kwenye viwango vya ubora vya FIFA kupata mechi za kirafiki za ushindani.
Kupitia mashidano haya timu zinapata nafasi ya kuongeza uzoefu na kuboresha nafasi zao katika viwango vya ubora vya FIFA.

