Simba Queens yajikita kileleni WPL

    Simba Queens imeendelea kujikita kileleni mwa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya watani wao wa jadi Yanga Princess.

    Mabao yote ya washindi katika mechi hiyo iliyofanyika tarehe 15 Mei katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam yalipatikana kipindi cha kwanza, mfungaji akiwa Jentrix Shikangwa.

    Yanga Princess ilibadilika kipindi cha pili kwa kufanya mashambulizi ya mara kwa mara na kufanikiwa kupata bao kupitia kwa Nabbosa Retticia.

    Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha wa Simba Queens Musa Mgosi aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kufuata maelekezo waliyopeana kwenye uwanja wa mazoezi.

    “Sisi kaulimbiu yetu ni tujitahidi tusishuke daraja, tukiwa na imani hii kaulimbiu imebeba kujituma zaidi kwenye kila mechi ili tushinde zote,” alisema Mgosi.

    Kocha Msaidizi wa Yanga Princess Said Maulid aliwapongeza Simba Queens kwa ubora waliouonesha huku akieleza ugumu walioupata mbele ya wapinzani wao hasa waliporuhusu kutanguliwa mabao 2-0.

    “Kwa mpira wa kike kutanguliwa kwa mabao 2-0 na mpinzani wako ni ngumu sana kurudi na kupata utulivu. Ilituchukua muda hadi tulipokwenda mapumziko.

    “Licha ya kupambana kipindi cha pili hatukufanikiwa kurudisha mabao yote, lakini walau tulipata lile moja,” alisema Kocha huyo.

    Mechi hiyo ndiyo iliyokamilisha
    raundi ya 16 ambapo matokeo ya mechi nyingine ni; Ruangwa Queens 0-0 Geita Queens, Alliance Girls 1-1 Tausi FC, Fountain Gate Princess 6-1 Bilo FC, Ceasiaa 1-0 Bunda Queens, Mashujaa Queens 0-0 JKT Queens.

    Share.