Mechi za hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB (CRDB Federation Cup) zitachezwa kati ya Mei 16 na 17 mwaka huu.
Upangaji huo wa ratiba ulifanywa moja kwa moja (live) leo kwenye Studio za Kituo cha Televisheni cha Azam, jijini Dar es Salaam.
Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Young Africans wamedondokea kwa JKT Tanzania watakaokuwa wenyeji kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ndiyo maskani ya robo fainali ya kwanza kati ya Coastal Union (Wagosi wa Kaya) na Singida Black Stars.
TRA United ambao wanacheza hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza watakuwa wageni wa Simba kwenye uga wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.
Kanda ya Magharibi imepata mechi ya robo fainali ambapo Mashujaa FC wataialika Azam FC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

