Ubingwa mlangoni kwa Simba Queens
Baada ya mzunguko wa 19 Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), timu ya Simba Queens imeendelea kuukaribia ubingwa baada ya sare 1-1 dhidi ya Tausi FC katika mechi iliyochezwa tarehe 27 Mei Uwanja wa KMC Complex.
Matokeo hayo yanaifanya Simba Queens kufikisha pointi 50, na rekodi ya kuwa ndio timu pekee ambayo haijapoteza mechi hadi sasa.
Simba Queens inazidi kuukaribia ubingwa kwa tofauti kubwa ya pointi kulinganisha na timu zinazofuatia kwenye msimamo.
Nafasi ya pili iliyoshikiliwa na Yanga Princess yenye pointi 43 huku JKT Queens ambao pia wana faida ya mechi moja mkonono wakiwa nafasi ya tatu kwa jumla ya pointi 42.
Wakati Yanga Princess ikiongeza pointi moja na kufikisha 43 baada ya kutoka suluhu na Fountain Gate Princesses, Maafande JKT Queens watakuwa wakiendelea kuwasubiri Ruangwa Queens kwa ajili ya kukamilisha hesabu za raundi hiyo.
Mechi nyingine zilizofanyika tarehe 27 Mei matokeo ni; Geita Queens 2-1 Bunda Queens, Mashujaa Queens 2–1 Ceasiaa Queens, Bilo FC 1-0 Alliance Girls.

