Tanzanite yazawadiwa milioni 50/

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan ameizawadia sh. milioni 50 timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite Queens) ikiwa ni sehemu ya pongezi kwa kufanikiwa kufuzu Kombe la Dunia 2026.

    Salamu hizo za pongezi kutoka kwa Rais ziliwasilishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda katika hafla maalum ya kuipongeza timu hiyo iliyofanyika hoteli ya Collina jijini Dodoma.

    “Tanzanite Queens mmelipa heshima Taifa, na mmetoa chachu kwa timu nyingine kuendelea kufanya vizuri.

    “Hivyo, Serikali inatambua mchango wenu na itaendelea kuwaunga mkono katika maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Poland mwezi Septemba,” alisema Waziri Makonda.

    Mbali na Waziri Makonda na viongozi wengine wa Serikali, hafla hiyo ilihudhuriwa na Rais wa TFF, Wallace Karia, Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, viongozi kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), na waandishi wa habari.

    Tanzanite Queens ilifuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa kuitoa Cameroon katika raundi ya nne ya mchujo.

    Share.