Kwa mara nyingine tena, timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) imeandika historia kwa kupanda kwa nafasi sita (6) kwenye viwango vya ubora vya FIFA vilivyotolewa Agosti 7, 2025, mafanikio ambayo yanadhihirisha ukuaji, juhudi na nidhamu ya hali ya juu ndani ya kikosi hicho kinachoiwakilisha Tanzania kwa fahari barani Afrika na kimataifa.

    Ikiwa imeweka rekodi kubwa kuwahi kutoka Afrika, Tanzania kupitia timu ya Twiga Stars imekuwa ndio timu pekee Kwa sasa kupanda kwa nafasi kubwa zaidi kutoka nafasi ya 131 hadi 137 huku ikiwa imefikisha alama 1096.

    Twiga Stars imekuwa na msimu mzuri katika ushiriki thabiti kwenye michezo ya kirafiki ya kimataifa (FIFA Calendar Matches) kwa kuzuia magoli mengi na kushambulia kwa kasi sambamba na kupata matoke mazuri kwenye mechi hizo.

    Aidha Twigastars imekuwa kwenye kiwango bora ukanda wa CECAFA hususani kwenye mashindano ya CECAFA Women’s Senior Championship yaliyofanyika Tanzania mwaka huu 2025 ambapo ilifanikiwa kubeba Ubingwa wa mashindano hayo.

    Ikiwa kwenye kiwango bora Twiga Stars imefanikiwa kufuzu kushiriki Fainali za WAFCON 2024 baada ya kupita miaka 9 na kuwa miongoni mwa timu 12 pekee Afrika kati ya Mataifa 54 kwenye Fainali zilizofanyika nchini Morocco mwaka huu 2025.

    Twiga Stars imekuwa kiigizo chema kwa timu nyingine za Taifa za Wanawake (Serengeti Girls U17, Tanzanite U20 na zile za U15 na U12) Kwa kupeperusha vyema bendera ya Taifa, si kwa maneno, bali vitendo uwanjani.

    Kupanda kwao ni ishara kuwa juhudi, nidhamu, na upendo kwa taifa unaweza kuleta mabadiliko makubwa,Tanzania imeamka kwenye soka la wanawake na dunia inaanza kusikia kelele ya Twiga Stars. Juhudi za kila mchezaji, kila kocha, kila mfanyakazi na hasa Kocha Mkuu Bakari Shime ambaye amekuwa na maono na nidhamu, akileta mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa uchezaji na maandalizi kama msingi imara wa kuwajenga mabinti hao.

    Hakika Twiga Stars ni fahari ya mabinti wa kitanzania hususani kwenye tasnia ya mpira wa miguu, kwani wengi wao wamefanikiwa kupiga hatua kubwa katika soka kupitia timu hiyo, lakini pia kuna vizazi vingi vya mabinti vinavyoandaliwa kwaajili ya kutumikia timu hiyo hapo baadae.

    Share.