Twiga, Malawi zatoshana nguvu
Mechi za kimataifa za kirafiki za kalenda ya FIFA zimemalizika leo Juni 6, 2026 kwa Twiga Stars kutoka suluhu na Malawi katika mechi ya marudiano iliyochezwa Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Katika mechi ya kwanza Twiga stars ilipata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Opa Clement katika dakika ya 48.
Akizungumza baada ya mechi kumalizika, Kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime alisema:
“Wapinzani walikua bora leo, lakini kikosi changu kilifanikiwa kuwazuia wasipate ushindi licha ya nafasi nyingi walizopata. Malawi ni timu nzuri na imetupa kipimo kizuri kuelekea katika mashindano ya WAFCON.”
Shime aliongeza kuwa katika mechi hizo ametoa nafasi kwa wachezaji chipukizi kupata uzoefu wa kucheza mechi za kimashindano.
Twiga Stars itashiriki Fainali za Kombe la mataifa Afrika kwa wanawake (WAFCON) zitakazofanyika nchini Morocco mwezi ujao ambapo imepangwa Kundi B pamoja na Afrika Kusini, Cote d’Ivoire na Burkina Faso.

