Twiga Stars, Malawi kujipima tena
Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) imejipanga kuhakikisha inapata ushindi kwenye mechi ya pili dhidi ya Malawi.
Mechi hiyi ya kirafiki ya kimataifa itachezwa Juni 6, 2026 Uwanja wa KMC, Dar es Salaam saa 10 kamili jioni.
Akizungumzia maandalizi, Kocha Msaidizi Edna Lema alisema wamejiandaa vizuri wakiwa na lengo la kupata ushindi mwingine dhidi ya Malawi.
“Licha ya kupata ushindi kwenye mechi ya kwanza, tulirudi uwanja wa mazoezi kufanyia kazi upungufu uliojitokeza ili kuhakikisha tunapata ushindi mwingine. Mechi hizi kwetu ni muhimu kama sehemu ya kujipima kuelekea Fainali za WAFCON 2026,” alisema Edna.
Amewataka Watanzania wajitokeze kwa wingi KMC kushuhudia nyota hao huku akisema hakutakuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi kutoka kile kilichocheza mechu ya awali.
Kwa upande wa Kocha wa Malawi, Lovemore Bazil alisema wamejipanga kwa ajiili ya mechi hiyo, na kikosi kitakuwa na mabadiliko kulinganisha na cha
mechi ya kwanza.
Alisema wamejipanga kupindua meza kwa kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Tanzania huku akifanya mabadiliko machache kwenye kikosi chake.
“Ninayo furaha kwa kikosi changu kwa kuonesha mchezo mzuri hapo mwanzoni, lakini pia tutakuwa na mabadiliko mawili au moja kwenye kikosi”, alisema Kocha Bazil.
Katika mechi ya kwanza iliyofanyika Juni 3, 2026 kwenye uwanja huo huo Twiga Stars ilishinda bao 1-0.

