Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Bakari Shime amesema mechi mbili za kirafiki kalenda dhidi ya timu ya Taifa ya Morocco zitaisaidia timu yake wakati ikijiandaa kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON).
Ikiwa nchini Morocco, Twiga Stars inacheza mechi mbili dhidi ya wenyeji; Aprili 13 na nyingine Aprili 18.
Akizungumzia mechi hizo mbili, Shime alisema kikosi chake kipo tayari baada ya kupata muda wa kuyafanyia marekebisho makosa yaliyojitokeza kwenye mechi ya kwanza ambapo kilipoteza mabao 3-0.
“Uchovu na makosa machache ya mchezaji mmoja mmoja ndio yalisababisha tupoteze, hivyo tumefanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi. Ninaamini vitu vingi vitabadilika kwenye mechi ya marudiano,” alisema Shime.
Pia alieleza kuwa baada ya maandalizi ya awali kabla ya Fainali hizo kusogezwa mbele timu hiyo haikupata mechi za kipimo sahihi, hivyo mechi dhidi ya Morocco imekuwa ni sehemu ya kupima utayari wa kikosi chake.
Twiga Stars imepangwa kundi ‘B’ Fainali za WAFCON 2026 zitakazofanyika nchini Morocco. Timu nyingine kwenye kundi hilo ni Afrika Kusini, Ivory Coast na Burkina Faso.

