Timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls) imetinga hatua ya pili ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Botswana.
Mechi hiyo ya marudiano imechezwa leo Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo wa nyumbani unaifanya Serengeti Girls kutinga raundi ya pili kwa jumla ya mabao 6-2.
Katika raundi ya pili, Serengeti Girls itacheza na Afrika Kusini Mei 2026. Afrika Kusini imeingia raundi hiyo baada ya timu ya Afrika ya Kati kujitoa katika mbio hizo za kufuzu Kombe la Dunia.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha wa Serengeti Girls, Bakari Shime alisema wana furaha kufuzu hatua ya pili ya mashindano.
“Wachezaji wameonesha kiwango bora. Hivyo tutaendelea na maandalizi kuhakikisha timu inapata ushindi dhidi ya Afrika Kusini.
“Afrika Kusini ni timu nzuri na mara nyingi imekua ikionesha ushindani wa hali ya juu. Tunakwenda kutengeneza timu ambayo itashindana na kupata matokeo yatakayotuweka katika nafasi nzuri ya kufuzu Kombe la Dunia,” alisema.
Mabao ya Serengeti Girls yalifungwa na Bahati Steven aliyetikisa nyavu mara mbili dakika ya 69 na 90 huku Harrier Juma akifunga moja dakika ya 84.

