Fainali ya utambuzi wa vipaji vya wachezaji wa mpira wa miguu waliopatikana katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa wasichana na wavulana imeanza Desemba 16, 2025.
Wachezaji 78 kutoka Kanda hiyo iliyojumuisha mikoa ya Iringa, Lindi, Mbeya, Mtwara, Njombe, Ruvuma, na Songwe wanashiriki katika fainali hiyo inayofanyika kwenye Kituo cha Ufundi cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Fainali hiyo ambayo ipo chini ya Stephen Morrow ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utambuzi wa Vipaji katika Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), na Kocha wa Vipaji anayetambuliwa na FIFA, Edward Munnelly inatarajia kukamilika Desemba 19.
Vipaji bora zaidi katika fainali hiyo, na pia fainali za Kanda zingine zitakazofanyika baadaye vitajumuishwa kwenye Programu ya Kuendeleza Vipaji (TDS) ya TFF ambayo inaendelea kwenye Kituo cha Ufundi cha TFF kilichopo Mnjanjani jijini Tanga.

