Timu ya Taifa ya Wanawake U20 (Tanzanite) imefuzu hatua inayofuata kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kuitoa Kenya kwa penalti 3-1.
Matokeo hayo ni baada ya mechi ya marudiano iliyochezwa Februari 14, 2026 Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam..
Dakika 90 za mechi hiyo zilipomalizika, ubao wa matokeo ulisoma Tanzanite 1, Kenya 0. Hivyo, matokeo ya jumla yakawa 1-1 baada ya Kenya kushinda mechi ya kwanza bao 1-0.
Mechi hiyo ilipokwenda hatua ya ‘matuta’ ndipo Tanzanite ikashinda kwa mikwaju ya penalti 3-1.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Tanzanite, Bakari Shime alisema licha ya kufuzu katika hatua inayofuata hakufurahishwa na kiwango cha wachezaji wake.
Aliwaomba radhi Watanzania na kuwataka kuwa na imani zaidi na mabinti hao kwenye hatua zinazofuata.
“Timu ya wakubwa Twiga Stars inaingia kambini kujiandaa kwa WAFCON kwa mwezi mmoja, hivyo tumejumuisha kikosi cha kwanza cha Tanzanite kwenye kambi hiyo.
“Lengo letu ni kuendelea kuwaweka sawa kuelekea mechi yetu inayofuata, alisema Shime.
Tanzanite imesalia na kibarua cha mwisho ili kukata tiketi ya Fainali ambapo inatarajia kukutana na Cameroon kwenye hatua hiyo.

