Ligi Kuu ya Wanawake yashika kasi
Mechi za Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) zimeendelea Desemba 17, 2025, kwa mzunguko wa tatu huku timu zikionesha ushindani mkubwa na vipaji vya kuvutia katika viwanja tofauti nchini.
Mechi zote zikipigwa majira ya saa 10:00 jioni, Bilo FC na Tausi FC walitoka suluhu, matokeo yaliyodhihirisha ugumu wa mchezo na uimara wa safu za ulinzi za timu zote mbili.
Bunda Queens waliibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Ruangwa Queens, walihitaji juhudi kubwa kuhakikisha pointi zote tatu zinabaki katika dimba la Karume pale mjini Musoma.
Katika mchezo mwingine wa kuvutia, Simba Queens wakiwa kwenye ardhi ya ugenini waliwaadhibu Fountain Gate Princess mabao 3-0. Mchezo huo ulipigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mjini Babati.
Mashujaa Queens walijipata nyumbani mbele ya Geita Queens baada ya mchezo wao kumalizika kwa ushindi wa mabao 4-1.
Kwa upande wa mabingwa watetezi JKT Queens wameendeleza heshima baada ya kuibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ceassia Queens, na kuendelea kujidhatiti kileleni mwa msimamo.
Huku Yanga Princess ikifunga hesabu kwa mchezo uliopigwa usiku Azam Complex, Dar es Salaam. Yanga Princess walionesha ubora wao kwa kuichapa Alliance Girls mabao 4-0.
Ligi hiyo itaingia mzunguko wa nne Desemba 22, 2025, huku kila timu ikiwa imepata muda wa kutafakari mwenendo wake.
Ends…

