Simba Queens yakabidhiwa Kombe
Timu ya wanawake ya Simba Queens leo Juni 12, 2026 imekabidhiwa rasmi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) baada ya kutwaa taji msimu wa 2025/26.
Sherehe za kukabidhiwa kombe hilo zimefanyika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam baada ya kukamilika mechi ya Ligi hiyo dhidi ya Alliance Girls, huku zikishuhudiwa na mashabiki, viongozi na wadau mbalimbali wa WPL.
Simba Queens walithibitisha ubingwa wao baada ya kufanya vizuri katika mechi za mwisho za msimu na kujikusanyia pointi 57 zilizowafanya kuongoza msimamo wa ligi.
Ikipoka ubingwa huo kutoka JKT Queens ambao hadi sasa wanapambana na Yanga Princess kuwania nafasi ya pili.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kombe hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Zubeda Sakuru aliwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki kwa mchango wao mkubwa ulioiwezesha timu kufikia mafanikio hayo.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo ni matunda ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na uongozi wa klabu hiyo.
Kwa kutwaa ubingwa wa msimu wa 2025/26, Simba Queens ndio timu itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa kwa ukanda wa CECAFA.
Timu nyingine pia zilikuwa uwanjani kukamilisha mzunguko wa 21 ambapo JKT Queens ilipata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Geita Queens, na matokeo mengine ni Mashujaa Queens 3-0 Bunda Queens, Yanga Princess 7-0 Bilo FC, Ruangwa Queens 0-1 Ceasiaa Queens, na Tausi FC wakitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Fountain Gate Princess.
Timu hizo zimebakiza mechi moja kukamilisha msimu wa 2025/2026.

