
Tanzania (Taifa Stars) haipo tena kwenye Fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoendelea nchini Morocco.
Wenyeji Morocco wameiondoa Stars katika 16 bora baada ya kushinda bao 1-0 kwenye mechi hiyo ya hatua hiyo iliyochezwa tarehe 4 Januari 2025 kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat.

Morocco ilibidi isubiri hadi dakika ya 63 kupata bao hilo pekee lililofungwa na Brahim Diaz.
Stars ilicheza vizuri mechi hiyo iliyokuwa na kasi kwa muda wote, huku Simon Msuva na Feisal Salum wakishindwa kutumia vizuri nafasi zilizopatikana katika kipindi cha kwanza.

Kabla ya mechi ya jana, Stars ilifanikiwa kufunga bao katika kila mechi ya hatua za makundi ingawa haikupata ushindi.
Wafungaji katika mechi hizo walikuwa Charles M’Mombwa (Nigeria 3-1), Simon Msuva (Uganda 1-1), na Feisal Salum (Tunisia 1-1).

Ikicheza Fainali hizo kwa mara ya kwanza mwaka 1980 jijini Lagos, Nigeria, Stars ilipoteza mechi mbili na sare moja katika hatua ya makundi, lakini ilifanikiwa kufunga bao katika kila mechi.
Mabao yote yalifungwa na mshambuliaji Thuwen Ally (Nigeria 3-1), (Misri 2-1), na (Ivory Coast 1-1).
Katika mechi ya Morocco, kikosi cha Stars inayonolewa na Miguel Gamondi, raia wa Argentina kiliundwa na;
Hussein Masalanga, Haji Mnoga/Shomari Kapombe , Mohamed Hussein, Ibrahim Hamad, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Alphonce Mabula/Idd Nado, Novatus Dismas, Feisal Salum, Seleman Mwalimu/Mbwana Samata, na Simon Msuva/Tarryn Allarakhia.


