Tanzanite hiyooo Kombe la Duni
Ni rasmi kuwa Tanzanite itakuwepo kwenye Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Septemba mwaka huu.
Fainali hizo za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa timu za Taifa za Wanawake chini ya miaka 20 zitafanyika nchini Poland.
Tanzanite imepata tiketi hiyo baada ya kuibandua Cameroon katika raundi ya nne ya mchujo Kanda ya Afrika.
Mechi ya uamuzi ilichezwa tarehe 10 Mei kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar ambapo Tanzanite iliifunga Cameroon mabao 2-0.
Tanzanite ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Yaounde kwa mabao 3-1, hivyo matokeo ya jumla (aggregate) kuwa 3-3.
Bao la ugenini la Tanzanite ndilo lililozitenganisha timu hizo. Winfrida Gerald ndiye aliyepachika bao hilo la ugenini dakika ya 27.
Mabao ya Tanzanite katika mechi hiyo ya marudiano yalipachikwa na Mary Aaron dakika ya saba, wakati la pili dakika ya 75 lilifungwa na Hasnath Ubamba.
Kikosi cha Tanzanite katika mechi hiyo chini ya Kocha Mkuu Bakari Shime kiliundwa na;
Nusrat Jaffar, Jamila Rajabu, Winfrida Gerald, Veronica Mapunda, Asha Omary, Diana Mnally, Hasnath Ubamba, Ester Maseke, Mary Aaron, Alia Fikiri, na Christer Basil.

