Serengeti Boys yafuzu Kombe la Dunia Qata
Tanzania (Serengeti Boys) imekuwa timu ya kwanza barani Afrika kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa wanaume chini ya miaka 17 zitakazofanyika baadaye mwaka huu nchini Qatar.
Serengeti Boys inayonolewa na Kocha Elieneza Nsanganzelu imefuzu baada ya tarehe 17 Mei kushinda mechi ya pili katika Fainali za Afrika (AFCON) zinazofanyika nchini Morocco kwa kuifunga Angola mabao 3-0.
Ushindi huo umeifanya Serengeti Boys kufikisha pointi sita na kuongoza kundi lake la C. Katika mechi ya kwanza Serengeti Boys iliichapa Msumbiji mabao 3-0.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Nsanganzelu alisema matokeo hayo yamepatikana kwa vile vijana wake walicheza kwa ubora.
Katika mechi dhidi ya Angola mabao ya Serengeti Boys yalifungwa na Razak Juma, Hassan Kizinga, na Sadam Hussein.
Afrika itawakilishwa na timu nane katika Fainali za Kombe la Dunia chini ya miaka 17 zitakazochezwa Qatar kuanzia tarehe 19 Novemba hadi tarehe 13 Desemba.
Hivyo, kila kundi kati ya manne yaliyopo kwenye AFCON litatoa timu mbili kuiwakilisha Afrika nchini Qatar.
Serengeti Boys ambayo tayari imefuzu robo fainali ya AFCON itakamilisha mechi za makundi kwa kucheza na Mali tarehe 20 Mei.

