Serengeti Boys yatinga fainali AFCON

    Timu ya Taifa ya Wavulana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) imeandika historia kwa kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kucheza Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

    Serengeti Boys imeingia hatua hiyo baada ya tarehe 28 Mei kuitoa Misri katika hatua ya nusu fainali ya Fainali hizo zinazofanyika nchini Morocco.

    Mechi hiyo iliyofanyika Kituo cha Ufundi cha Mohammed VI ilimalizika suluhu katika muda wa kawaida. Hatua iliyofanya mikwaju ya penalti kuamua mshindi ambapo Serengeti Boys ilishinda 4-3.

    Issa Chole wa Serengeti Boys alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi, hivyo kujishindia tuzo inayotolewa na mdhamini mkuu wa Fainali hizo kampuni ya Total Energies.

    Mchezaji huyo pia alipata tuzo hiyo kwenye mechi ya hatua ya makundi dhidi ya Msumbiji.

    Mechi fainali dhidi ya Senegal itafanyika tarehe 2 Juni kuanzia saa 1 kamili jioni.

    Share.