CECAFA U17 yaanza kwa kishindo

    Mashindano ya CECAFA kwa wanawake chini ya miaka 17 yameanza kwa kishindo katika Uwanja wa KMC, Dar es Salaam huku ikishuhudiwa mvua ya kwenye mechi ya ufunguzi.

    Mechi hiyo ilikua kati ya Kenya na Sudan ambapo Kenya ilishinda mabao 16-0. Hata hivyo, dakika ya 51 mwamuzi alilazimika kumaliza mechi hiyo baada ya wachezaji zaidi ya watano wa Sudan kuumia na kushindwa kuendelea na mechi hiyo.

     

    Mechi ya pili ilikuwa kati ya Tanzania na Somalia ambapo Tanzania iliibuka na ushindi wa mabao 4-0.

     

    Mabao ya Tanzania (Serengeti Girls) yalifungwa na Yasinta Michael (dakika ya kwanza), Bahati Steven dakika ya 36 na 61, na Fatuma Shagembe dakika ya 54.

     

    Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Msaidizi wa Serengeti Girls, Ester Chabruma alisema:

     

    “Lengo la timu ni kushinda kila mechi ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kutwaa Kombe la CECAFA mwaka huu. Nawapongeza wachezaji wangu kwa kuanza vizuri kwenye mechi ya kwanza.”

     

    Mashindano ya CECAFA yataendelea tena Juni 14, 2026 kwa mechi mbili za Kundi B kupigwa katika Uwanja wa Azam Complex ambapo Sudan Kusini itacheza na Zanzibar saa 7.00 mchana wakati Uganda akijiuliza mbele ya Djibouti saa 10.00 jioni.

    Share.