Yanga, Coastal kucheza nusu fainali Kombe la CRDB
Timu za Coastal Union na Yanga zitacheza mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Mechi hiyo itachezwa tarehe 20 Mei katika Uwanja utakaotangazwa baadaye na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Coastal Union ndiyo iliyokuwa ya kwanza kukata tiketi ya nusu fainali baada ya kuifunga Singida Black Stars mabao 4-2 katika mechi iliyochezwa tarehe 16 Mei.
Katika mechi hiyo iliyofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, hadi dakika 90 zinakamilika timu hizo zilitoka suluhu. Mikwaju ya penalti ndiyo iliyotumika kuamua mshindi.
Nayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania katika robo fainali nyingine iliyofanyika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.
Robo fainali ya tatu (Simba na TRA United), na ya nne kati ya Mashujaa na Azam zitachezwa tarehe 17 Mei mwaka huu.
Mashujaa itaikabili Azam kuanzia saa 10 kamili jioni katika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, wakati ile ya Simba na TRA United itachezwa KMC Complex kuanzia saa 12.30 jioni.

