Afya maji rasmi Taifa Star
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeisaini mkataba wa miaka miwili na kampuni ya kutengeneza vinywaji baridi ya Watercom.
Mkataba huo wa miaka miwili kupitia maji chapa ya Afya kwa timu zote za Taifa umesainiwa tarehe 26 Mei 2026 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba huo, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema wamekuwa wakifanya kazi na kampuni hiyo kwa muda mrefu ambapo kwa sasa wameona ni wakati sahihi kwa pande hizo mbili kuingia makubaliano rasmi.
“Ni muda mrefu wamekuwa wakitusaidia ingawa haikuwa rasmi. Lakini sasa tunaamini huu ndio wakati sahihi kufanya kazi pamoja.
“Leo tutasaini mkataba hapa wa miaka miwili na kampuni hii kuwa ndio mdhamini wetu rasmi wa maji ya kunywa. Naamini utatusaidia sana katika kuendesha shughuli za timu za Taifa hasa kwa kipindi hiki ambacho timu zetu nyingi zipo kwenye maandalizi ya mashindano mbalimbali,” alisema Rais Karia.
Naye Meneja Masoko wa Watercom, Mohamed Salim alisema wanayo furaha kushirikiana na TFF, huku akitoa pongezi kwa kazi kubwa ya kusimamia na kuendesha shughuli za mpira wa miguu inayofanywa na Shirikisho hilo.
“Tuna furaha leo kwa kuingia rasmi makubaliano yetu ya kurasimisha ushirikiano kati yetu wa kuwa na haki ya kutoa huduma ya vinywaji baridi kwa timu zote za Taifa.
“Tuna imani kupitia mkataba huu tutakuwa na mchango mkubwa kwa TFF katika kufanikisha baadhi ya majukumu kwa timu za Taifa hasa zinapokuwa kambini,” alisema Salim.
Mkataba huo kupitia chapa ya Afya kwa timu zote za Taifa unakadiriwa kuwa na thamani ya sh. milioni 70.

