Michuano ya NBC Youth League imeendelea kwa kishindo mzunguko wa tatu, huku mechi za Kundi A na Kundi B zikichezwa katika viwanja mbalimbali nchini.

    Katika mechi hizo umeshuhudiwa ushindani mkubwa, pamoja na mabao ya kuvutia.

    Katika Kundi A, timu ya JKT Tanzania ilionesha ubora wake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3–0 dhidi ya Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

    Nayo timu ya TRA ikiwa nyumbani katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora ililazimishwa mbele ya Simba SC.

    Katika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, timu ya Mashujaa FC ilipata ushindi wa kusisimua wa mabao 3–2 dhidi ya KMC FC ‘Kino Boys’.

    Mchezo mwingine wa Kundi A uliochezwa Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, uliwakutanisha Pamba Jiji na Dodoma Jiji, ambapo timu hizo zilitoka sare ya 2–2.

    Kwa upande wa Kundi B, timu ya Mtibwa Sugar iliibuka na ushindi wa mabao 2–0 dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

    Azam FC ikiwa nyumbani Azam Complex Chamazi, ilipata ushindi mnono wa mabao 5–1 dhidi ya Tanzania Prisons.

    Nayo Namungo FC ilipata ushindi mwembamba wa bao 1–0 dhidi ya Coastal Union ‘Wana-Mangushi’ katika Uwanja wa Majaliwa.

    Mchezo wa mwisho wa mzunguko wa tatu uliwakutanisha wenyeji Young Africans SC, ambao waliibuka na ushindi wa mabao 3–1 mbele ya Fountain Gate FC katika Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha TFF, Dar es Salaam.

    Ligi hiyo ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 inaingia raundi ya nne kwa mechi zitakazochezwa katika viwanja mbalimbali.

    Ends….

    Share.