Serengeti Girls yaendeleza vipigo CECAFA

    Timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 17 (Serengeti Girls) imezidi kung’ara kwenye mashindano ya CECAFA baada ya tarehe 15 Juni kupata ushindi mnono wa mabao 10-0 dhidi ya Sudan katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

     

    Serengeti Girls imekuwa na mwendelezo mzuri katika mashindano hayo baada ya kupata ushindi katika mechi zote mbili ilizocheza mpaka sasa.

     

    Bahati Steven ndiye aliyeng’ara zaidi katika mechi hiyo baada ya kufunga mabao matano. Mabao mengine yalifungwa na Mirembe John, Sundy Masasila na Harrier Juma aliyefunga matatu.

     

    Akizungumza baada ya mechi, Kocha wa Serengeti Girls, Ester Chabruma alisema ilikuwa nzuri na wachezaji wameonesha kiwango bora.

     

    “Tunajipanga kwa ajili ya mechi ya mwisho dhidi ya Kenya ambao tunafahamu itakuwa ngumu kutokana na ubora wa kikosi chao,” alisema Ester.

     

    Serengeti Girls itacheza mechi ya mwisho ya hatua ya makundi na Kenya tarehe 18 Juni kwenye Uwanja wa KMC kuanzia saa kumi kamili jioni.

    Share.