Mechi 6 za Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL) mzunguko wa nne zilizochezwa Desemba 22, 2025 zimekamilika kwa timu ya Yanga Princess kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

    Yanga Princess waliotumia uwanja wa Azam Complex kama wenyeji wa mechi yao dhidi ya Geita Queens walishinda mabao 5-0 , matokea yaliyobadili upepo wa vinara JKT Queens walioshuka hadi nafasi ya tatu.

    Ushindi wa Yanga Princess umeiweka kileleni kwa tofauti ya mabao dhidi ya Simba Queens iliyopo nafasi ya pili.

    Simba Queens wenyewe wakiwa na pointi 12 walipata ushindi wa bao 1-0, ugenini dhidi ya Ceasiaa Queens. Hiyo ni mechi ya nne mfululizo kwa Ceasiaa kupoteza ikiwa haina pointi yoyote katika nafasi ya kumi na moja.

    Mechi nyingine ilipigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mjini Babati ambapo JKT Queens ililazimishwa sare ya 1-1 mbele ya Fountain Gate Princess.

    Mashujaa Queens waliotumia uwanja wa Kituo cha Ufundi TFF kilichopo Kigamboni walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Alliance Girls.

    Hata hivyo mzunguko huo umekuwa mzuri kwa Bilo FC baada ya kuutumia vyema Uwanja wa Nyamagana kwa kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Ruangwa Queens. Bilo FC sasa imefanikiwa kuongeza pointi hadi nne ikiwa nafasi ya saba, huku Ruangwa Queens ikiwa ya nane na pointi tatu.

    Mchezo kati ya Bunda Queens na Tausi ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

    Mzunguko unaofuata wa Ligi hiyo utachezwa kati ya Desemba 27 na 28 mwaka huu.

    Ends…

    Share.