Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) iliyopo kambini nchini Misri inaendelea na matayarisho kwa ajili ya Fainali za WAFCON 2026 zitakazofanyika Machi mwaka huu nchini Morocco.
Twiga Stars imewekeza nguvu kwenye utimamu wa mwili kwa wachezaji ikiwa pia ni maandalizi ya mashindano ya ‘Pink Ladies’ ambayo ni sehemu ya mwisho ya matayarisho ya Fainali hizo.
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shime amesema timu hiyo itakuwa na kambi ya wiki mbili nchini Misri kabla ya kwenda Dubai.
İkiwa Dubai itashiriki mashindano ya Pink Ladies ambayo yatashirikisha nchi nne za Ghana, Hong Kong, Russia na Tanzania.
“Dhamira yetu ni kufanya kitu kikubwa kwenye Fainali za WAFCON, hivyo kambi hii na mashindano madogo ya Dubai naamini yatatusaidia kurekebisha upungufu tulioubaini msimu uliopita.
“Baada ya kujifanyia tathmini kutoka hatua tuliyomaliza mwaka jana, tumejidhatiti kufanya marekebisho makubwa ili kuhakikisha tunakwenda kufanya vizuri awamu hii,” alisema Shime.
Fainali za WAFCON zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi Machi 17, 2026 huku Tanzania ikipangwa kundi moja na nchi za Burkina Faso, Afrika Kusini na Ivory Coast.

