BetaTQ mshirika wa TFF kwenye data
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesaini mkataba wa haki za data na dijitali (Data rights and Digitalization ) za Ligi Kuu na kampuni ya BetaTQ.
Mkataba huo umesainiwa tarehe 21 Aprili jijini Dar es Salaam katika hafla iliyoongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani na Ofisa Mtendaji Mkuu wa BetaTQ, Neithan Swed.
Akizungumza katika hafla hiyo, Nyamlani alisema kupitia makubaliano hayo, TFF linakabidhi rasmi haki zote za data za Ligi Kuu kwa BetaTQ.
Alisema hatua hiyo ni uwekezaji wa kimkakati katika mustakabali wa mpira wa miguu nchini, na itakuwa ni fursa kwa wachezaji kuanza kuonekana kimataifa kupitia data hizo, na ushindani baina ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu nchini.
“Kwa miaka mingi tumeijenga soka yetu kwa vipaji, juhudi na mapenzi ya mashabiki. Lakini ukweli ni kuwa dunia imebadilika, soka ya kisasa haitegemei tena macho pekee. Inategemea data, uchambuzi na teknolojia,” alisema Nyamlani.
Naye Swed alisema wanalenga zaidi kujenga mfumo imara utakaoleta thamani halisi ya mpira wa miguu.
Alisema wamebuni mifumo ya kisasa inayochakata na kusimamia data kwa viwango vya kimataifa. Mifumo hiyo ni Soka Metrics na Metrics Eye ili kuweka msingi wa kisasa wa kusimamia, kuchambua, na kukuza soka nchini.
Mfumo huo utafanya kazi kwa kushirikiana na teknolojia ya Generative AI na wataalamu wa kibinadamu ili kuhakikisha data inakuwa sahihi, inaaminika na inatumika kwa ufanisi.
Alisema wametengeneza data center kubwa itakayowezesha uhifadhi na uchambuzi wa taarifa kwa kiwango cha juu, huku binadamu wakibaki kuwa sehemu muhimu ya mchakato wa uthibitishaji na ubora wa data hizo.

