Mpira rasmi wa Ligi Kuu ya NBC 2025/2026 watambulishwa
Kampuni ya Just Fit sports Gear kwa kushirika na TFF pamoja na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara imezindua mpira rasmi (Official Match Ball) utakaotumika katika michezo yote ya Ligi Kuu NBC kwa msimu huu wa 2025/2026.
Tukio hilo limefanyika katika makao makuu ya Kampuni ya Just Fit Sports Gear iliyopo Masaki, Dar es laam.
Akizungumza wakati wa tukio hilo Makamu wa Kwanza wa rais TFF, Athuman Nyamlani alisema, Ni jambo kubwa na la kihistoria kwa Tanzania kuweza kuwa na mpira maalumu ambao utatumika katika michezo ya Ligi msimu huu.
” Ni mpira wenye ubora ambao umekidhi viwango vinavyohitajika na umezingatia uhalisia wa viwanja vyetu. Jambo hili linazidi kuupa thamani mpira wa Tanzania na ni mategemeo yetu kama shirikisho kuendeleza mazungumzo na Just Fit ili kuona namna ya kuzidi kuwekeza katika maeneo mengine” alisema Nyamlani.
Naye msemaji wa kampuni ya Just Fit Hadji Degigo amesema ni fahari kwao kama kampuni kuwa sehemu ya kuendelea kukuza mpira wa Tanzania kupitia uwekezaji walioufanya katika eneo la vifaa kwa waamuzi na kutengeneza mpira rasmi utakaotumika katika Ligi ya NBC.
“Mpira huu umetengenezwa hapa Tanzania kwa kutumia malighafi yakwetu ambayo ina uwezo wa Kudumu muda mrefu lakini pia mpira huu una uwezo wa kuchezeka kiurahisi katika mazingira na hali yoyote ya hewa ikiwemo mvua”. Alisema Degigo
Tukio hilo la utambulisho wa mpira rasmi wa Ligi ya NBC lilihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa rais TFF Athuman Nyamlani, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ACPA Ibrahim Mwayela, Mkurugenzi Mkuu wa Just Fit sports Gear Salim Salim na wadau wengine wa mpira.



