Tanzania Yaanza kwa Ushindi Mchezo wa Kwanza “Kufuzu Kombe la Dunia 2026”
Timu ya Taifa ya wanawake U20 (Tanzanite Queens ) imeanza vyema kampeni za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi mbele ya Angola kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Septemba 21, 2025 katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Kipindi cha kwanza cha mchezo huo timu ya Tanzania ilianza kwa utulivu mkubwa huku ikiwasoma zaidi wapinzani wake ambao kabla ya hapo hawakuwahi kukutana nao.
Kadri dakika songa mbele ndivyo ambavyo timu ya Tanzanite ilikuwa iliongeza jitihada za kusaka bao la kutangulia na la ushindi.
Juhudi hizo za upambanaji zilizofanywa na wachezaji wa Tanzanite ziliza bao la kuongoza lililofungwa na Winfreda Gerald kwa mkwaju wa penati baada ya Diana Mnary kufanyiwa madhambi ndani ya boxi
Mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko timu ya Taifa ya Tanzanite ilikuwa Iko mbele kwa magoli 2-0 yote yakifungwa na Winfrida Gerald.
Kipindi cha pili cha mchezo huo, sambamba na mabadiliko yaliyofanyika kwa timu ya Tanzanite, mambo yalizidi kuwa mazuri baada ya kuongeza magoli mawili zaidi yote yakifungwa na Hasnath Ubamba na kufanya mchezo huo kumalizika Tanzanite ikibakiza alama zote tatu muhimu nyumbani.
Akizungumza baada ya mchezo huo Kocha Mkuu Bakari Shime alisema matokeo ya mchezo huo yamewapatia mwanga zaidi na matumaini ya kuendelea kupambana zaidi ili kuweza kusonga mbele kwenye harakati hizo za kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.
“Tumekuwa na mchezo mzuri, tumetengeneza nafasi nyingi ambazo baadhi tulizitumia vizuri na nyingine zilipotea kutokana na makosa kwenye safu ya ushambuliaji,” alisema Shime.
Aidha, Kocha Shime aliongeza kwa kusema kuwa pamoja na benchi lake la ufundi watakwenda kufanyia kazi makosa yote ili kuhakikisha kutokujirudia kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa Septemba 27,2025 huko Angola.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji Diana Mnary alisema wamefurahia matokeo hayo huku akiahidi kwenda kupambana zaidi kwenye mchezo wa marudiano.
“Tunamshukuru Mungu kwa ushindi huu, kwani licha ya kupata upinzani mkubwa kutoka kwa wapinzani wetu, hawakuwa kikwazo kwetu kuweza kutimiza kile tulichoelekezwa na makocha wetu,” alisema Mnary
Tanzanite sasa inajipanga na mchezo wa marudiano utakaopigwa Septemba 27, 2025 nchini Angola, huku ikiwaaubiri kati ya Ethiopia au Kenya endapo itafanikiwa kusonga mbele kwenye mkondo unaofuata.

