Timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 (Serengeti Girls) imeanza vyema michuano ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Botswana.
Mechi hiyo imechezwa tarehe 10 Aprili, saa 10 jioni katika Uwanja wa Obed Itani Chilume nchini Botswana.
Serengeti Girls ilianza mechi hiyo kwa kasi na kupata mabao yote matatu kipindi cha kwanza. Bao la mapema lilifugwa dakika ya 15 na Fatuma Hassan huku la pili likifungwa na Bahati Steven dakika ya 40, na Christer Basil akipachika la tatu dakika ya 45.
Wenyeji Botswana walipata bao dakika ya 42 kabla ya kuongeza bao la pili kwa mkwaju wa penati mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Baada ya mechi kumalizika, Kocha wa Serengeti Girls, Bakari Shime alisema licha ya ushindi huo, bado wana kazi ya kufanya kwenye mechi ya marudiano.
Mechi ya marudiano itachezwa tarehe 19 Aprili 2026 jijini Dar es Salaam.
Mshindi wa jumla kati ya Tanzania na Botswana atacheza hatua inayofuata dhidi ya Afrika Kusini.

