Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua rasmi mpango wa kuuza kwa mnada haki za kibiashara za betting kwa mashindano mbalimbali yanayosimamiwa na shirikisho hilo, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuongeza mapato na kuvutia wawekezaji kwenye tasnia ya soka.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, mnada huo utahusisha mashindano makubwa nchini, ikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania Bara, michezo ya timu za taifa, Kombe la Shirikisho (Federation Cup), ligi za wanawake, na Ligi Daraja la Kwanza.

    TFF imesema hatua hiyo inalenga kuongeza uwazi na ushindani wa kibiashara, pamoja na kuhakikisha soka la Tanzania linapata hadhi ya juu katika masoko ya kimataifa. “Tunataka kujenga mfumo endelevu wa mapato ambao utasaidia kuboresha mashindano, kulipa waamuzi kwa wakati, na kuwekeza katika maendeleo ya wachezaji chipukizi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

    Kupitia mpango huu, wadau wa sekta ya michezo na makampuni ya betting yanayoendesha shughuli kisheria nchini wanapewa nafasi ya kipekee kushirikiana na TFF katika kukuza thamani ya mashindano na kuongeza mapato yatakayorejeshwa kwenye maendeleo ya soka.

    Mnada wa haki hizi unatarajiwa kuendeshwa kwa uwazi chini ya usimamizi wa kitaalamu, huku TFF ikiahidi kutoa taarifa za kina kuhusu washindi wa zabuni na masharti ya mikataba.

    Share.