Ni mwendelezo wa michuano ya CRDB Federation Cup hatua ya raundi ya 16 bora itakayoanza kutimua vumbi tarehe 10 Aprili 2026.

     

    JKT Tanzania dhidi ya Mbuni FC, wakitarajia kuchanga karata zao Dar es Salaam kwenye dimba la Meja Jenerali Isamuyo, Geita Gold na Mashujaa FC watakuwa wakijipambanua kutafuta nafasi ya kusonga mbele katika dimba la Nyankumbu. Mechi zote zikipigwa saa 10:00 jioni.

     

    Akizungumzia matayarisho ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Mbuni FC, Leonard Budeba, alisema wamefika salama Dar es Salaam na wamepata mechi za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa, huku akiweka wazi ubora wa wapinzani wao JKT Tanzania sambamba na kuwa na wachezaji bora.

     

    Alisema kikosi chake kipo tayari kuwakabili na kutafuta matokeo mazuri akiwa na imani na baadhi ya wachezaji wenye uzoefu wa kucheza Ligi Kuu.

     

    Kwa upande wa nahodha wa Mbuni FC, Pascal Robat, amesema kikosi kiko vizuri kiafya na morali ipo juu huku wakilenga kucheza na timu tatu za Ligi Kuu ambapo kesho watakuwa wanacheza na timu ya pili.

     

    Naye kocha wa JKT Tanzania, Ahmed Ally, alisema wanakwenda kukutana na timu inayocheza ligi tofauti lakini wao wanapambana kufikia malengo waliyojiwekea.

     

    Alisema watacheza kwa ubora wao huku akisisitiza umuhimu wa kujenga ari ya wachezaji kuelekea mchezo huo, hasa baada ya kutoka kucheza na Namungo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya NBC.

     

    Kwa upande wa mchezaji wa JKT Tanzania, Gamba Iddy, amesema wamejiandaa vizuri kuelekea mchezo huo mgumu wa kesho na wako tayari kupambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

     

    Mechi nyingine za hatua hiyo zitazikutanisha Young Africans vs TMA Stars na Coastal Union vs Pamba Jiji tarehe 11 Aprili 2026 na nyingine ni Namungo vs TRA United Uwanja wa Majaliwa, Simba SC vs Dodoma Jiji.

     

    Mechi nyingine ya Dar es Salaam, Azam FC vs Fountain Gate na Singida Black Stars wakiwakaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Airtel, zote zikipigwa Aprili 12, 2026.

    Share.