Timu ya Taifa “Taifa Stars” kupitia kocha mkuu Hemedi Suleiman Morocco ameweka wazi kuwa timu yake imejipanga vilivyo kuuendea mchezo wa mwisho kukamilisha hatua ya makundi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (Central Africa Republic) Agosti 16, 2025.

    Mchezo huo wa nne kwa Stars kwenye michuano ya CHAN 2024 unatarajiwa kuchezwa majira ya saa 1:00 usiku Benjamin Mkapa, ambapo Mashujaa hao watashuka Dimbani huku wakiwa wamekwisha kukata tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali baada ya kukusanya alama 9 Kwa kushinda mechi 3 za awali.

    Akizungumzia maandalizi kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Agosti 15, 2025 Benjamin Mkapa kocha wa Taifa Stars Hemed Suleiman “Morocco”, amesema kikosi chake kipo tayari kuhakikisha kinamaliza hatua ya makundi ya michuano ya CHAN kwa kishindo kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

    Morocco alisema dhamira yao ni kumaliza hatua ya makundi wakiwa kileleni na rekodi ya kushinda michezo yote, kama walivyopanga tangu mwanzo wa mashindano.

    “Tangu tulipoanza maandalizi ya mashindano haya, tulijiwekea malengo mawili makubwa – kushinda kila mechi na kumaliza tukiwa vinara wa kundi. Hatujapanga kupoteza hata mchezo mmoja, na kesho tunataka kuthibitisha hilo.Kila mchezo tumekutana na upinzani mkali, lakini wachezaji wameonyesha nidhamu ya hali ya juu na ari kubwa ya kushinda. Hii ndiyo sababu tunaamini tunastahili tulipo sasa”. Alisema Morocco

    Aidha aliongeza kwa kusema kuwa mashabiki wamekuwa silaha muhimu kwa mafanikio ya kikosi hicho huku akisisitiza wajitokeze kwa wingi kwenye mchezo huo, akiamini kwamba shangwe zao ndizo zinazo wapa nguvu za ziada uwanjani.

    Ikumbukwe Stars iliyopo kundi ‘B’ ndio timu ya kwanza kutangulia hatua ya robo fainali huku ikiwa imeweka rekodi ya kushinda mechi zake zote za awali hatua ya makundi.

    Share.