Kocha Miguel Gamondi amethibitishwa rasmi leo Februari 16, 2026 kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) katika hafla ya utiaji saini mkataba iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Utiaji saini wa mkataba huo kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), na Kocha huyo ulishuhudiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda.
Raia huyo wa Argentina atakinoa kikosi cha Stars kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kukaimu nafasi hiyo kwa muda, na kukiongoza kikosi hicho kutinga hatua ya 16 bora katika Fainali za AFCON 2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Makonda alisema, Serikali imeridhia ombi la kumlipa mshahara Kocha wa Stars, na inaendelea kufanya uwekezaji katika kuboresha miundombinu kwa ajili ya Fainali za AFCON 2027.
“Kupitia uwekezaji huu nina imani kikosi cha Stars kitafanya vizuri katika mashindano ya AFCON na kuliwakilisha taifa la Tanzania vizuri. Niipongeze TFF kwa kazi nzuri wanayoifanya, mpira wa Tanzania upo katika viwango vya juu na ni matamanio yetu kuendelea kufanya vizuri zaidi kimataifa,”alisema Makonda.
Naye Kocha Gamondi alisema: “Ni furaha na heshima kwangu kuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars ninapenda mpira na ninaipenda Tanzania.
“Naamini tukishirikiana tutauweka mpira wa Tanzania katika viwango bora Afrika.”
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, Rais wa TFF, Wallace Karia na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Oscar Mirambo.

