Bingwa mtetezi wa mashindano ya Shule Afrika ya CAF (African Schools Football Championship- ASFC) timu ya taifa ya wavulana U15 imeanza maandalizi ya kutetea ubingwa kwenye fainali zitakazofanyika Harare, Zimbabwe.
Mashindano hayo yataaanza Aprili 2-10, 2026 yakijumuisha timu 16 kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambazo zimegawanywa katika makundi mawili ya wasichana na wavulana.
Akizungumzia fainali hizo, Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania, Boniface Pawasa alisema:
“Sitarajii mashindano kuwa rahisi kwa mwaka huu kutokana na ubora wa timu shiriki. Tunakwenda kupambana ili kulinda heshima ya Tanzania.”
Timu shiriki kwa upande wa wavulana ni mwenyeji Zimbabwe, Benin, Morocco, Senegal, Uganda, Zambia, DR Congo na bingwa mtetezi Tanzania.
Upande wa wasichana ni Zimbabwe, Burkina Faso, Morocco, Guinea, Tanzania, Zambia, DR Congo pamoja na Ghana ambaye ni bingwa mtetezi.
Tanzania ilitwaa ubingwa wa Afrika baada ya kuifunga Senegal kwa mikwaju ya penaltı 3-2 baada ya kutoka suluhu Aprili 26, 2025 nchini Ghana na kutwaa tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo ya mchezaji bora na timu yenye nidhamu.

